WAFANYAKAZI 58 WA VITUO VYA KULELEA WATOTO WADOGO MCHANA WAPATA MAFUNZO YA MALEZI SONGEA
Na Albano Midelo,Songea
WAFANYAKAZI 56 wa vituo vya kulelea Watoto wadogo mchana wilayani
Songea mkoani Ruvuma wameanza mafunzo ya siku tano kwenye ukumbi
wa Anglikana mjini Songea.
Mafunzo hayo yameratibiwa na Ofisi ya Rais TAMISEMI na kusimamiwa na
Idara ya Ustawi wa Jamii Mkoa wa Ruvuma ambapo wawezeshaji wa
mafunzo hayo ni Taasisi ya ANJITA ambayo imepewa Mamlaka ya kutoa
mafunzo hayo.
Mgeni rasmi kwenye ufunguzi wa mafunzo hayo,Afisa Ustawi wa Jamii
Mkoa wa Ruvuma Victor Nyenza amesema katika Mkoa wa Ruvuma kuna
vituo 138 vya kulelea Watoto wadogo mchana na kwamba kati ya vituo
hivyo ni vituo 68 tu ndiyo vimesajiriwa.
Ametoa rai kwa vituo ambavyo bado havijasajiriwa kuhakikisha wanavisajiri
vituo vyao na kwamba ifikapo Januari 2024 vituo vyote viwe vimesajiriwa
vinginevyo vitafungwa.
Amesema wafanyakazi wote waliohudhuria mafunzo hayo watapewa cheti
cha kuhitimu baada ya kumaliza mafunzo na kwamba wote ambao
wameanzisha vituo ambavyo havijasajiriwa wataambanisha cheti
walichopata mafunzo ili kupata usajiri.
“Hatutarajii katika Mkoa wa Ruvuma kuwa na kituo cha kulelea Watoto
mchana ambacho hakisajiriwa na kina walezi wa Watoto wasiokuwa na
sifa ya mafunzo elekezi kwa vitendo,vituo ambavyo vitakuwa havina sifa
tutakwenda kuvifunga kwa mujibu wa sheria’’,alisisitiza Nyenza.
Amesisitiza kuwa mafunzo hayo ni muhimu kwa walezi wa watoto kwa
kuwa wanakwenda kupata mbinu na stadi mbalimbali za kuboresha na
kuimarisha malezi ya Watoto wanaohudumiwa.
Amesisitiza kuwa vitendo vingi vya ukatili wa Watoto na matukio mengi ya
utekaji na utelekezaji wa Watoto yanafanyika pia kwenye vituo vya kulelea
Watoto wadogo na kwamba Watoto wengi wanatekwa wakiwa katikati ya
kituo cha malezi na nyumbani hivyo ameagiza kila kituo kiwe na rejesta ili
kusaidia wamiliki wa vituo kujiweka upande salama.
Amelitaja jukumu la walezi wa Watoto wadogo mchana kuwa ni
kumwandalia mazingira wezeshi mtoto ili aweze kukua vizuri na kuelewa
stadi tatu za kusoma,kuandika na kuhesabu.
Akizungumza kwenye ufunguzi wa mafunzo hayo Mratibu wa mafunzo
kutoka Taasisi ya ANJITA Janeth Malela amezitaja mada ambazo
zitafundishwa kwenye mafunzo hayo kuwa ni sayansi ya dhana ya malezi
,makuzi na maendeleo ya awali ya mtoto uanzishaji na usimamizi wa vituo
vya Watoto na vifaa vya kujifunzia na kuchezea Watoto.
Mada nyingine amezitaja kuwa ni mbinu za ujifunzaji na kuelewa Watoto
kuanzia miezi sita hadi miaka sita,afya lishe na usafi wa mazingira,ulinzi na
usalama kwa mtoto,utambuzi wa mapema na afua stahiki kwa Watoto
wenye mahitaji maalum,namna ya kufanya tathmini ya maendeleo ya mtoto
na mafunzo kwa vitendo.
Baadhi ya wafanyakazi wa vituo vya kulelea watoto wadogo mchana kutoka wilaya ya Songea wakipata mafunzo ya malezi ya watoto yaliyoratibiwa na Ofisi ya Rais TAMISEMI na kusimamiwa na Idara ya Ustawi wa Jamii Mkoa wa Ruvuma na kufanyika kwa siku tano kwenye ukumbi wa Kanisa Anglikana mjini Songea.
Afisa Ustawi wa Jamii Mkoa wa Ruvuma Viktor Nyenza akizungumza wakati anafungua mafunzo ya wafanyakazi wa vituo vya kulelea watoto wadogo wilaya ya Songea kwenye ukumbi wa kanisa Anglikana Songea.
Post a Comment