Header Ads

test

KAMATI ZA MAAFA MKOA ZAJENGEWA UWEZO WA KUZUIA ,KUJIANDAA NA KUKABILIANA NA MADHARA YA EL-NINO

 

NA, MWANDISHI WETU

Kamati za maafa Ngazi ya Mkoa zajengewa uwezo juu Kuimarisha Uwezo wa Kuzuia na Kujiandaa Kukabiliana na Madhara ya mvua za El-nino kufuatia utabiri wa mwelekeo wa mvua za msimu wa Vuli kwa kipindi cha mwezi Oktoba hadi Desemba, 2023 kuonesha uwepo wa El-Niño itakayosababisha vipindi vya mvua kubwa kwa mwezi Oktoba mpaka Disemba 2023 na kuendelea mpaka Mwezi Januari 2024.

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa kikao kazi cha utekelezaji wa Mpango wa Kuimarisha Uwezo wa Kuzuia na Kujiandaa Kukabiliana na Madhara ya mvua za El-nino kwa Kamati ya Usimamizi wa Maafa mkoa wa Morogoro 
Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Sera, Bunge na Uratibu Mhe. Ummy Nderiananga amesema kuwa, Serikali ilianza kutekeleza hatua za kuzuia madhara haya toka mwezi Julai 2023 wakati taarifa ya awali ya dalili za uwezekano wa uwepo wa El Nino ilipotolewa na Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania.

Kikao kazi hichi kinafanyika kwa siku mbili kuanzia tarehe 25 hadi 26 septemba, 2023 na kuhusisha wajumbe wa Kamati ya Usimamizi wa Maafa ngazi ya Mkoa wakiwemo; Wakuu wa Wilaya, Katibu Tawala wa Mkoa, Wakurugenzi wa Halmashauri, Wenyekiti wa Halmashauri pamoja na washiriki kutoka washiriki kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, wawezeshaji kutoka Idara ya Menejimenti ya Maafa Ofisi ya Waziri Mkuu, Jeshi la Zimamoto na Uokoaji, Jeshi la Polisi Tanzania, TMA na DarMAERT Pamoja na Wawakilishi wa Taasisi mbalimbali na Viongzozi wa dini.

Alisema kuwa zoezi hilo limefanyika kwa mikoa 14 inayopata misimu miwili ya mvua kwa mwaka ambayo ni Kagera, Geita, Mwanza, Shinyanga, Kusini mwa mkoa wa Simiyu, kaskazini mwa mkoa wa Kigoma, Dar es Salaam, Tanga, Pwani (ikiwemo visiwa vya Mafia) na kaskazini mwa mkoa wa Morogoro.


“Kikao kimezingatia wajibu mlio nao kwa mujibu wa Sheria ya Usimamizi wa Maafa namba 6 ya Mwaka 2022 na Kanuni zake, ambayo imeanzisha Kamati za Usimamizi wa Maafa za Mikoa, Wilaya, Kata na Vijiji au Mitaa. Jukumu la msingi la Kamati hizi ni kuchukua hatua kwa lengo la kuzuia na kupunguza madhara ya majanga ya aina zote na kujiandaa kukabili na kurejesha hali kwa ubora zaidi endapo maafa yatatokea.” alisisitiza Mhe. Nderiananga.

Naibu Waziri aliongezea kuwa, kazi hiyo imezingatia uwajibikaji wa pamoja ambapo, Ofisi ya Waziri Mkuu imeshirikiana na Wizara za kisekta na Taasisi za Serikali na Wadau kuendelea kuimarisha hatua ambazo zinaendelea kuchukuliwa na Mamlaka za Mikoa na Serikali za Mitaa katika Mikoa husika.

Ametumia nafasi hiyo kuzikumbusha kamati za maafa zote kuendelea kujiandaa na kukabili maafa nchini kwa kuimarisha mifumo ya utendaji, rasilimali zilizopo huku wakitambua masuala ya menejimenti ya maafa ni jukumu la kila mmoja hivyo upo umuhimu wa kuunganisha nguvu ya pamoja.

“Ni jukumu letu sote katika nafasi zetu kama wajumbe wa Kamati za Usimamizi wa Maafa kutekeleza kimamilifu hatua za kuchukua katika sekta zenu kwa kuzingatia kuwa madhara yanaweza kuongezeka endapo hatua stahiki hazitachukuliwa kwa wakati. Natarajia kuwa baada ya kikao kazi cha leo, Kamati hasa ngazi ya Halmashauri zote za Mkoa zitaimarisha utekelezaji wa hatua za kuzuia madhara ili kuhakikisha tunaokoa maisha na mali kwa ustahimilivu wa taifa,”alisema.

Alizikumbusha Taasisi zinazohusika kuendelea kuwa mstari wa mbele wakati wa tukio la maafa zinapaswa kujiandaa kikamilifu kwa kuweka utaratibu wa pamoja ikiwa ni pamoja na kuwa na mpango wa dharura wa utendaji na utaratibu wa mawasiliano wakati wa dharura ili ziweze kuchukua hatua kwa haraka na ufanisi ili kuokoa maisha.

“Taasisi hizo ni pamoja na zile zinazohusika na huduma ya utafutaji na maokozi, usalama wa wananchi, afya na makazi ya muda na huduma zingine za kijamii. Aidha, taasisi zinazohusika kutoa huduma wezeshi au saidizi pamoja na kuimarisha mifumo kama vile usafiri, mawasiliano, nishati na maji zinakumbushwa kujiimarisha ili kuhakikisha shughuli za kijamii na kiuchumi haziathiriki wakati wa maafa. Taasisi saidizi zina wajibu wa kuwezesha taasisi zenye jukumu ongozi katika kuokoa maisha na mali ili zitekeleze majukumu kwa ufanisi pamoja na kupunguza athari kwa jamii”,Alisisitiza

Sambamba na hilo aliwaeleza kuwa hatua hiyo ni muhimu ili kuhakikisha juhudi zinazochukuliwa na Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, katika kuimarisha uchumi na huduma za kijamii katika ujenzi wa Taifa letu zinakuwa stahimilivu dhidi ya maafa.

Ni dhahiri kuwa hatua zinazochukuliwa zitachangia katika juhudi zake katika kuongoza na kusimamia utekelezaji wa mipango ya Serikali pamoja na maelekezo ya Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi 2020-2025 kwa manufaa makubwa kwa wananchi na tija iliyokusudiwa.

“Ilani ya Chama Cha Mapinduzi ya mwaka 2020 hadi 2025 kuhusu masuala ya Menejimenti ya maafa nchini kifungu cha 107, kinaeleza katika kipindi cha miaka mitano ijayo, Chama Cha Mapinduzi kitaendelea kuhakikisha Serikali inaendelea kusimamia kikamilifu vyombo vinavyoshughulika na maafa kuwa na mpango wa utayari wa kuzuia, kujiandaa, kukabili na kurejesha hali haraka pindi maafa yanapotokea kwa kuchukua hatua mbalimbali” alibainisha Mhe. Nderiananga.

Kwa upande wake Mkuu wa wilaya ya Malinyi Mhe. Sebastian Waryuba akimwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Morogoro ameeleza kuwa mkoa umejiandaa katika kukabiliana na maafa na kueleza wataendelea kutoa elimu kwa umma juu ya uwepo wa mvua hizo huku akitahadharisha wakazi wa Malinyi kuendelea kuchukua tahadhari kwa kuzingatia ni maeneo yanayoathiriwa na maafa ya mvua mara kwa mara.

Naye, Mkuu wa Wilaya ya Morogoro Mhe. Rebeca Nsemwa ametahadharisha wakazi wa maeneo yanayoathiriwa kwa wingi, kuendelea kuzingatia ushauri wa wataalam ikiwemo kuhama maeneo hatarishi na kutotupa taka zinazosababisha kuziba kwa mifereji ya maji na kuimarisha kingo zote.



Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Sera, Bunge na Uratibu Mhe. Ummy Nderiananga akihutubia wakati wa ufunguzi wa kikao kazi cha utekelezaji wa Mpango wa Kuimarisha Uwezo wa Kuzuia na Kujiandaa Kukabiliana na Madhara ya mvua za El-nino kwa Kamati ya Usimamizi wa Maafa mkoa wa Morogoro kilichofanyika Ukumbi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Morogoro tarehe 25 Septemba, 2023.

Mkuu wa wilaya ya Malinyi Mhe. Sebastian Waryuba akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Morogoro kuhusu hali ya maafa katika mkoa huo na namna mkoa ulivyojipanga kukabili maafa wakati wa kikao kazi cha utekelezaji wa Mpango wa Kuimarisha Uwezo wa Kuzuia na Kujiandaa Kukabiliana na Madhara ya mvua za El-nino kwa Kamati ya Usimamizi wa Maafa mkoa wa Morogoro.

Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Menejimenti ya Maafa Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu) Luteni Kanali Selestine Masalamado akizungumza jambo wakati wa wa kikao kazi cha utekelezaji wa Mpango wa Kuimarisha Uwezo wa Kuzuia na Kujiandaa Kukabiliana na Madhara ya mvua za El-nino kwa Kamati ya Usimamizi wa Maafa mkoa wa Morogoro.



Wajumbe wa kikao kazi cha utekelezaji wa Mpango wa Kuimarisha Uwezo wa Kuzuia na Kujiandaa Kukabiliana na Madhara ya mvua za El-nino kwa Kamati ya Usimamizi wa Maafa mkoa wa Morogoro wakifuatilia kikao hicho.

Mkuu wa wilaya ya Malinyi Mhe. Sebastian Waryuba akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Morogoro akizungumza jambo kwa Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Sera, Bunge na Uratibu Mhe. Ummy Nderiananga mara baada ya kuwasili mkoani humo kwa lengo la kufungua kikao kazi cha kikao kazi cha utekelezaji wa Mpango wa Kuimarisha Uwezo wa Kuzuia na Kujiandaa Kukabiliana na Madhara ya mvua za El-nino kwa Kamati ya Usimamizi wa Maafa mkoa wa Morogoro.


(PICHA ZOTE NA OFISI YA WAZIRI MKUU)

No comments