Header Ads

test

MALAWI YAIPONGEZA TANZANIA MASUALA YA MENEJIMENTI YA MAAFA.

NA. MWANDISHI WETU

Serikali ya Jamhuri ya Malawi imekabidhi tuzo kwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kutambua mchango wake wakati wa maafa ya Kimbunga Freddy kilichotokea Machi, 2023 nchini humo.

Tuzo hiyo iliyokabidhiwa na Mkuu wa Chuo cha Ukamanda na Unadhimu Jeshi la Ulinzi la Malawi Brigedia Jen. Luke Mwetseni wakati walipotembelea nchini wakiwa na wanafunzi na wakufunzi kutoka Chuo hicho kwa lengo la kubadilishana uzoefu na kujifunza namna Tanzania inavyosimamia masuala ya menejimenti ya maafa.

Akizungumza mara baada ya kukabidhiwa rasmi, Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Sera, Bunge na Uratibu Dkt. Jim Yonazi ameishukuru Serikali ya Jamhuri ya Malawi kwa kutambua mchango uliotolewa wakati nchi hiyo ilipopata maafa yaliyosababishwa na Kimbunga hicho huku akisema Tanzania itaendelea kuimarisha mahusiano yaliyopo kati yao kwa kuzingatia kuwa masuala ya maafa yanaweza kutokea kwa taifa lolote kutokana na sababu mbalimbali.

“Tumeipokea tuzo hii kwa heshima na tunatoa shukrani nyingi kwa namna mlivyojali na tunaahidi kuendelea kuimarisha umoja na mshikamano kati yetu na Malawi pamoja na Nchi nyingine.Kipekee tunampongeza Rais wetu Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuimarisha diplomasia na mataifa mengine,” Alisisitiza Dkt. Yonazi

Aliongezea kuwa, hatua hiyo imeipa nchi heshima huku akiwakaribisha kujifunza zaidi masuala ya menejimenti ya maafa na kutembelea vivutio vilivyopo nchini.

Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu) Dkt. Jim Yonazi akiangalia tuzo iliyotolewa na Serikali ya Jamhuri ya Malawi kwa kutambua mchango wa Serikali ya Tanzania ilipotoa misaada ya kibinadamu wa Maafa ya Kimbunga Freddy kilichotokea Machi 2023 nchini huo.

No comments