Header Ads

test

UJENZI WA KM 25 ZA LAMI, MAINGILIO YA DARAJA LA SIBITI UPO MBIONI KUANZA: BASHUNGWA

 

Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa amesema kuwa ujenzi wa barabara ya maingilio katika Daraja la Sibiti zenye urefu wa kilometa 25 kwa kiwango cha lami tayari umeanza na upo katika hatua za awali za utelelezaji.

Ujenzi wa barabara hiyo wenye  kilometa 5 upande wa Wilaya ya Meatu na Kilometa 20  upande wa Wilaya ya Mkalama ni kiungo muhimu kwani zitaaunganisha mikoa ya Singida na Simiyu.

Bashungwa ameeleza hayo Oktoba 6, 2023 mkoani Singida wakati alipofika kukagua daraja la Sibiti (mita 82) ambalo ujenzi wake umekamilika na kumtambulisha mkandarasi wa Kampuni ya CHICO ambaye atatekeleza barabara za maingilio.

Amesema kuwa ujenzi wa barabara hiyo ni muhimu katika shughuli za kiuchumi na kijamii kwa mikoa ya Arusha, Manyara, Singida na Simiyu.

Sambamba na hilo, Bashungwa ameeleza Dira ya Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kuboresha mtandao wa barabara ambapo jumla ya kilometa 2,035 za barabara kwa kiwango cha lami zinatarajiwa kujengwa  na tayari mikataba ya ujenzi wa barabara hizo zimeshasainiwa kwa utaratibu wa EPC + F.

"Moja ya mkakati wa Mhe. Rais katika kuongeza ufanisi katika Sekta ya usafirishaji ni pamoja na kuamua kuijenga barabara ya Karatu - Mbulu - Haydom - Sibiti - Ng'amhuzi (Meatu) - Lalago - Maswa (km 389)” amesema Bashungwa

Bashungwa ameeleza kuwa Serikali ipo katika hatua za kumpata mkandarasi wa kuijenga kwa kiwango cha lami barabara ya Iguguno - Nduguti - Sibiti - Gumanga - Chemchem (km 89) mara baada ya usanifu wake kukamilika  mkoani Singida

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Miradi kutoka Wakala wa Barabara (TANROADS) Mha. Boniface Mkumbo amesema mradi huo utatekelezwa na mkandarasi CHICO na kusimamiwa na TECU kwa gharama ya Shilingi Bilioni 21.776

Ameongeza kuwa muda wa utekelezaji wa mradi ni miezi 18 ikijumuisha miezi 3 ya maandalizi na unatarajiwa kukamilika ifikapo mwezi Februari, 2025.

Mha. Mkumbo amesema kuwa sehemu ya barabara hiyo ni mchepuo wa barabara kuu kusini ma Serengeti inayoanzia Karatu - Mbulu - Haydom - Sibiti - Ng'amhuzi (Meatu) - Lalago - Maswa ambayo yenye urefu wa kilometa 389.




No comments