Header Ads

test

RAIS SAMIA ATOA BILIONI 40 KUTEKELEZA MIRADI YA ELIMU RUVUMA

 

Na Albano Midelo,Songea

RAIS Dkt.Samia Suluhu Hassan ametoa shilingi bilioni 40 kwa ajili ya
kutekelezaji miradi mbalimbali katika sekta ya elimu mkoani Ruvuma.
Hayo yamesemwa na Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Kanali Laban Thomas
wakati anatoa taarifa ya utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi Mkuu wa CCM
kwa kipindi cha Julai hadi Desemba 2022 na Januari hadi Juni 2023
kwenye ukumbi wa Parokia ya Bombambili mjini Songea.

Akizungumzia sekta ya elimu Kanali Thomas amesema katika kipindi hicho
sekta ya elimu ilipokea shilingi bilioni 7.7 kujenga shule mpya za sekondari
katika Halmashauri zote nane zilizopo mkoani Ruvuma.

“Ujenzi huu unajumuisha shule za sekondari za kata kumi zilizogharimu
shilingi bilioni 4.7,shule ya sekondari mpya ya wasichana ya Mkoa
iliyopewa jina la Dkt.Samia Suluhu Hassan iliyojengwa wilayani Namtumbo
kwa gharama ya shilingi bilioni 4.1’’,alisema.

Ameongeza kuwa sekta ya elimu pia ilipokea fedha za ujenzi wa mabweni
saba ya wanafunzi wa shule za msingi na sekondari kwa gharama ya
shilingi milioni 640 na ujenzi wa vyumba vya madarasa 792 vya elimu ya
msingi na sekondari vilivyogharimu shilingi bilioni 14.93.

Kwa mujibu wa Mkuu wa Mkoa,Rais Samia pia katika sekta ya elimu
ametoa shilingi milioni 250 kujenga shule mpya ya msingi katika kitongoji
cha Lizaboni Halmashauri ya wilaya ya Songea.

Ameongeza kuwa serikali imetoa fedha zaidi ya shilingi bilioni mbili
kukamilisha vyumba vya madarasa 121 vya shule za msingi na sekondari
Pamoja na maabara 23 za shule za sekondari kupitia fedha za Tozo na
Serikali Kuu.

Kulingana na Mkuu wa Mkoa,katika sekta ya elimu Rais Samia pia ametoa
shilingi bilioni 3.12 kwa ajili ya ujenzi wa vyumba 156 vya madarasa katika
shule za sekondari mkoani Ruvuma hali iliyosababisha kuondoa kabisa
tatizo la upungufu wa vyumba vya madarasa.

Mkuu wa Mkoa ameongeza kuwa walimu wote wa shule za msingi na
sekondari wapatao 9,079 katika Mkoa wa Ruvuma wamegawiwa
vishikwambi kwa ajili ya uboreshaji wa ufundishaji.

Mkoa wa Ruvuma una jumla ya shule za msingi 841 na shule za sekondari
233
Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Kanali Laban Thomas
Jengo la utawala katika shule mpya ya sekondari Luhira Manispaa ya Songea ambapo serikali imetoa shilingi milioni 470 kupitia program ya SEQUP ambapo katika Mkoa wa Ruvuma kupitia programu ya SEQUIP serikali imetoa shilingi bilioni 7.7 kujenga shule mpya za sekondari.




Majengo ya utawala na baadhi ya vyumba vya madarasa katika shule ya sekondari ya wasichana Mkoa wa Ruvuma iliyojengwa wilaya ya Namtumbo na kupewa jina la Dkt.Samia Suluhu Hassan ambapo serikali imetoa shilingi bilioni 4.1 kutekeleza mradi wa ujenzi wa shule hiyo yenye uwezo wa kuchukua wanafunzi zaidi ya 1000 wa kidato cha kwanza hadi cha sita.Tayari shule hiyo imeanza kuchukua wanafunzi wa kidato cha Tano kuanzia mwaka huu.

No comments