Header Ads

test

Waziri Jafo atembelea Alliance One akiapa kulinda viwanda nchini

 

Na mwandishi Wetu, Morogoro


Waziri wa Viwanda na Biashara Dk Suleman Jafo, ameahidi kuvilinda viwanda vyote nchini ili
viendelee kutoa ajira kwa vijana na hivyo kuwapunguza presha baada ya kumaliza elimu ya
juu na ya kati.

Ameyasema hayo wakati alipotembelea Kampuni ya Alliance One, ambayo inamiliki kiwanda
cha kuchakata tumbaku kilichopo eneo la Kingolwira katika Manispaa ya Morogoro.
Dk Jafo aliyekuwa kwenye ziara ya siku moja mkoani humo, ambapo amepokelewa na
Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni hiyo Ephraim Mapoore, amepokea changamoto kadhaa
za kampuni hiyo, ikiwemo ya ukosefu wa maji pamoja na mkanganyiko wa ujenzi wa
miundombinu ya umeme kati ya kampuni hiyo na shirika la umeme nchini Tanesco.

Nimeambiwa kwamba mlijenga line maalum ya kuwaletea umeme hapa kiwandani kwa
makubaliano maalum na Tanesco kwa gharama ya takribani shilingi 1bn, kwa maana ya
kurejesha fedha hizo kwenye matumizi yenu ya kila mwezi,lakini umeibuka utata ambao
unaendelea kwa miaka miwili sasa" amesema.

Amesema, ameambiwa pia kuhusu changamoto ya maji iliyopo kiwandani hapo, ambapo
kwa miaka yote wanatumia maji ya mvua ambayo wanayovuna wao wenyewe na
kuyahifadhi kwenye mabwawa, huku wakiwa hawana miundombinu ya maji kutoka
mamlaka ya maji ya manispaa ya Morogoro,(Moruwasa) licha ya kuomba kuletewa huduma
hiyo kwa miaka mingi lakini bila mafanikio.

Nimezichukua changamoto zote hizi na mimi hili ni jukumu langu kubwa kuhakikisha kero
zote za viwanda zinaisha, na kwakweli nawapongeza sana kwa mambo mnayofanya,
ikiwemo kodi nyingi mnazolipa na gharama za bidhaa kama umeme mnazolipa ndizo
zinazoendeleza mashirika mengi ya serikali nchini," amesema.

Waziri Jafo pia ameipongeza kampuni hiyo ambayo ilianzishwa mwaka 1998, ambapo hadi
sasa imetoa ajira nyingi kiwandani hapo zikiwemo ajira 208 za wafanyakazi wa kudumu na
zingie 3500 za muda mfupi.

Aidha Waziri Jafo amewaasa viongozi wa kampuni hiyo kuhakikisha kuwa wanalipa kodi zote
halali,huku akiahidi kuchukua mapendekezo ya kampuni hiyo kuhusu utitiri wa kodi
zinazofanana kwenye sekta ndogo ya tumbaku.

Msemaji wa Kampuni hiyo Wakili John Magoti katika wasilisho lake lililojumuisha kero hizo,
alisema kampuni hiyo ambayo imewekeza kiwandani hapo mtaji wa shilingi bilioni 182,
inashirikiana na jumla ya vyama vya msingi vya ushirika 150, vyenye jumla ya wanachama
13,000 kwenye kilimo cha mkataba wa tumbaku walioko kwenye mikoa ya
Kigoma,Tabora,Shinyanga na Mara.

“Kiwanda chetu kina uwezo wa kuchakata kilo milioni 80 kwa muda miezi 7,kikiwa na uwezo
wa kuhifadhi kilo milioni 64 kwa wakati mmoja,” alisema na kuongeza kuwa mwaka huu

kampuni yake imenunua kilo milioni 26 yenye thamani ya shilingi bilioni 162 ambazo zote
zimewafikia wakulima.

Amesema kampuni yake inalipa ni mlipaji mzuri wa kodi za nchi pamoja na michango
mbalimbali ya kisheria zikiwemo kodi ya zao ambapo kwa mwaka huu pekee kampuni
imelipa shilingi bilioni 4.2 ambazo zimelipwa kwenye halmashauri ambazo zinalima zao hilo.
“Kampuni yetu inalipa kodi mbalimbali ikiwemo kodi mapato isiyopungua shilioni 2.6,
tunalipa pia kodiya ujuzi,kodi ya zuio,tunatoa michango yote stahiki kwenye vyama vya
kutumbaku vikiwemo Wetcu,Latcu,Katcu,Cetcu n.k” alisema

Kuhusu maslahi ya wafanyakazi amesema kampuni yake inawajali wafanyakazi ambapo
inawalipa misharaha na stahiki zingine kwa wakati wakati, akitolea mfano kwamba kwa
miaka mitano mishahara pamoja na maslahi mengine ni jumla ya shilingi bilioni 41.5 huku
michango ya wafanyakazi hao kwenye mifuko ya hifadhi za jamii ikiwa ni jumla ya shilingi
bilioni 2.1.

Amesema kampuni yake inatoa misaada kwa jamii katika maeneo matatu ambayo ni
afya,elimu na mazingira ambapo kila mwaka inatenga shilingi milioni 400.

Awali Kaimu Mkurugenzi wa Kiwanda cha kampuni hiyo Shepherd Karuwa amesema
kampuni hiyo ilingia kwenye mkanganyiko na Tanesco kutokana na makubaliano ya
kutengeneza miundombinu ya umeme kuanzia eneo la Msamvu mpaka kiwandani hapo kwa
makubaliano maalum,ambayo kwa sasa yameingia kwenye mgogoro kwa miaka miwili sasa.
“Tulikubaliana kwamba tujenge miundombinu ya umeme kwa gharama zetu lakini kwa
kutumia wakandarasi wao na kazi hiyo ilikamilika na ilisimamiwa na wao wenyewe” alisema.

Amesema kwamba kwa mujibu wa mkataba wa makubaliano hayo ambao Tanesco
wameshindwa kuutekeleza, kampuni ilikuwa kuwa inarejesha gharama zake kwa kulipia
asilimia sitini ya matumizi ya sasa, huku asilimia 40 ikienda kwenye gharama za ujenzi wa
miundominu hiyo.

“Lakini sasa Mheshimiwa kinachoendelea wakati huu sisi tunalipa bili yetu yote na wao
Tanesco wamegoma kutulipa pesa yetu, na tukisema labda tuanze kukata pesa yetu kidogo
kwenye gharama za umeme tuliotumia sawasawa na mkataba wao wanatutishia kutuzimia
umeme kiwandani”amesema.

Amesema kwamba gharama za matumizi ya umeme ambazo Alliance One wanailipa Tanesco
ni kiasi cha shilingi milioni 200, ambapo matumizi yao ya umeme ni megawati 3.5.

Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni ya tumbaku ya Alliance One Ephraim Mapoore(katikati) akimfafanulia jambo Waziri Jafo namna madaraja ya zao hilo yalivyo baada ya kuichakata.Anayeshuhudia ni Mkuu wa Wilaya ya Morogoro Rebecca Msemwa
Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni Alliance One Tobacco Tanzania Limited, Ephraim Mapoore (kulia)akifafanua jambo kuhusu uchakataji wa tumbaku kwa Waziri wa Viwanda na Biashara Dk Selemani Jafo(Wa Pili kulia), wakati waziri huyo alipotembelea kiwanda cha kampuni hiyo kilichopo Kingolwira manispaa ya Morogoro jana. Wa pili Kushoto ni Msemaji wa Kampuni hiyo Wakili Joh Magoti.
Meneja wa Uchakataji wa Kampuni ya tumbaku ya Alliance One Jimmy Mollel(kulia) akimfafanulia Waziri wa Viwanda na Biashara Dk Selemani Jafo namna uchakaji ulivyo,huku Msemaji wa Kampuni hiyo Wakili John Magoti akishuhudia
Meneja Upokeaji Tumbaku wa Kampuni Alliance One Tobacco Tanzania Limited, Elizabeth Chuma akifafanua jambo kwa Waziri wa Viwanda na Biashara Dk Selemani Jafo(Katikati), wakati waziri huyo alipotembelea kiwanda cha kampuni hiyo kilichopo Kingolwira manispaa ya Morogoro jana. Kushoto ni Msemaji wa Kampuni hiyo Wakili Joh Magoti.
Waziri Jafo akiwa katika ofisi za kampuni ya Alliance One akipitishwa kwenye wasilisho maalum la kampuni hiyo na Mkurugenzi wa Alliance One Ephraim Mapoore

No comments