Header Ads

test

RUVUMA WAJADILI UZALISHAJI WA ZAO LA SOYA NA AFYA YA UDONGO

 


Wadau wa kilimo, wakulima, na wataalam wa upimaji wa udongo kutoka Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI) wamefanya kikao  cha kujadili uzalishaji wa zao la soya na upimaji afya ya ndogo  kilichofanyika kwenye  Ukumbi wa Cottage Heritage mjini Songea.

 Katibu Tawala wa Mkoa wa Ruvuma Ndugu Mary Makondo amefungua kikao hiko na kueleza namna serikali ilivyotoa kipaumbele katika sekta ya kilimo na jinsi ilivyojipanga kuongeza uzalishaji wa mazao na bidhaa za kilimo.

"Serikali imejipanga kuongeza uzalishaji, uchakataji na usafirishaji nje wa mazao ya kilimo na kugawa vitendea kazi kwa Maafisa ugani."alisema

 Katibu Tawala huyo amewaagiza wakuu wa Idara kuendelea kusimamia zoezi la upimaji wa udongo na kuhakikisha maafisa ugani wanatekeleza malengo yaliyokusudiwa.

Naye Mtafiti wa Udongo kutoka TARI, Watson Matamwa, amesema hadi sasa afya ya udongo imepimwa  Zaidi yay a mikoa 15 na kwamba udongo wa Mkoa wa Ruvuma umepungua rutuba na eneo kubwa la kilimo lina  udongo wenye asidi  nyingi, hali ambayo inasababisha kupungua kwa uzalishaji wa mazao.

Matamwa ameitaja Halmashauri ya Madaba wilayani Songea kuwa ina udongo wenye asidi kwa kiasi kikubwa, hali inayosababisha kuongezeka kwa matumizi ya mbolea na kushindwa kufikia malengo ya uzalishaji yaliyowekwa na serikali.

Mtafiti huyo ameeleza tayari wameshatoa elimu kwa wakulima kutumia chokaa ili kukabiliana na hali hiyo na kulitaja zao la Soya kama moja ya mazao muhimu katika kuboresha afya ya udongo

 Magnus Ndunguru mmoja wa wakulima walioshiriki kikao hicho, ameeleza kuwa elimu waliyoipata itawasaidia kuboresha shughuli zao za kilimo na ameiomba serikali kuendelea kuwawezesha wakulima kwa kuwasaidia kupata mitaji

Sanjari na hayo Kikao hicho kimejadili mwenendo wa Soko la zao la Soya na namna mfumo wa stakabadhi za ghala unavyosimamiwa katika Mkoa wa Ruvuma.
Kulia ni Katibu Tawala wa Mkoa wa Ruvuma Ndugu Mary Makondo akizungumza kwenye kikao cha wadau wa kilimo cha kujadili zao la soya na upimaji wa afya ya udongo kilichofanyika kwenye ukumbi wa Heritage Coltage mjini Songea ,kushoto ni Kaimu Katibu Tawala wa Uchumi na Uzalishaji Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Deo Sibula
Baadhi ya wadau wa kilimo kutoka katika Halmashauri za Mkoa wa Ruvuma wakiwa kwenye kikao cha wadau wa kilimo

No comments