Header Ads

test

BASHUNGWA -SERIKALI IPO MBIONI KUJENGA DARAJA MZINGA KUONDOA KERO YA MSONGAMANO WA MAGARI BARABARA YA DAR-KILWA

 

Mwamvua Mwinyi, Mkuranga Oktoba 23, 2024

Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa ameeleza serikali ipo mbioni katika mchakato wa kutangaza zabuni kwa ajili ya ujenzi wa daraja la Mzinga, linalotarajiwa kupunguza changamoto ya msongamano wa magari katika barabara inayounganisha Dar es Salaam na Kilwa.
Aidha, serikali inakusudia kupanua barabara ya Mbagala Rangi Tatu - Vikindu hadi Mwanambaya, hatua ambayo itaondoa kero ya foleni inayosababisha usumbufu kwa watumiaji wa barabara hiyo kwa sasa.

Akizungumza Oktoba 23, 2024, wakati wa ziara yake maalum mkoani Pwani, wilayani Mkuranga, Bashungwa alisema kuwa serikali ya awamu ya sita inaendelea kutenga mabilioni ya fedha kwa ajili ya kuboresha miundombinu ya barabara na madaraja.

"Serikali inatambua changamoto ya msongamano huo na iko kwenye mchakato wa kutatua tatizo hilo ili kupunguza foleni," alisisitiza Bashungwa.

Kuhusu barabara ya Mkuranga-Bandari ya Kisiju, ambayo imejengwa kwa kiwango cha lami chini ya Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) Mkoa wa Pwani, Waziri alibainisha kuwa barabara hiyo ni muhimu kwa kukuza uchumi wa eneo hilo.

" Rais Samia Suluhu Hassan kufunganisha Bandari na baadhi ya barabara, nitafikisha umuhimu wa kuiweka barabara hii katika mkakati wa vipaumbele vya maendeleo, ili kuiunganisha Bandari na barabara kwa kiwango cha lami "

Katika ziara hiyo, Waziri alizindua daraja la barabara ya Mwanambaya-Mipeko (Mto Mzinga), lililojengwa na Wakala wa Barabara za Mijini na Vijijini (TARURA).

Alimshukuru Rais Samia kwa kuiwezesha TARURA kuunganisha mikoa ya Dar es Salaam na Pwani.

Pia, alimuelekeza Meneja wa TARURA Mkoa wa Pwani, Leopard Runji, kupeleka mahitaji ya kutatua changamoto za miundombinu ya eneo hilo wizarani ili zitafutiwe ufumbuzi kupitia bajeti ya Mfuko wa Barabara.

Awali, Meneja wa TANROADS Mkoa wa Pwani, Mhandisi Baraka Mwambage, alitoa taarifa kuhusu barabara ya Mkuranga-Bandari ya Kisiju na kusema inajengwa kwa awamu, ambapo kilomita 6 zimekamilika, na inatafutiwa fedha kwa ajili ya kumalizia kilomita 1.02, ambayo inakadiriwa kugharimu sh. bilioni 7.17.

Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Alhaj Abubakar Kunenge, alifafanua barabara hizo ni kichocheo muhimu cha maendeleo ya uchumi wa eneo hilo.



 

No comments