Header Ads

test

TPF Net PWANI WAKABIDHI MSAADA KWA WANAFUNZI WA MANDELA SEK WALIOUNGULIWA BWENI

Mwenyekiti wa TPF Net Mkoa wa Pwani, Mrakibu Mwandamizi wa Polisi (SSP) Batseba Kassanga ameongoza maafisa, wakaguzi, na askari wa vyeo mbalimbali kukabidhi msaada wa mashati 70 kwa wanafunzi wa kike wa Shule ya Sekondari Mandela, Wilaya ya Kipolisi Chalinze, ambao bweni lao liliungua moto mnamo Oktoba 12, 2024.

Akizungumza wakati wa kukabidhi msaada huo, SSP Batseba aliwapa pole uongozi wa shule na wanafunzi kwa janga hilo, akiwaomba walichukulie kama ajali na kuchukua tahadhari  dhidi ya majanga ya aina hiyo.

Mkuu wa Polisi wa Wilaya ya Kipolisi Chalinze, Mrakibu Mwandamizi wa Polisi (SSP) Sophia Lyidenge, aliwasihi wanafunzi hao kusoma kwa bidii zaidi kutokana na kipindi kifupi kilichobaki kuelekea mitihani yao ya mwisho.

Alisisitiza umuhimu wa kudumisha nidhamu watakapokuwa nyumbani wakisubiri matokeo, ili wasiharibu ndoto zao.

Mwanafunzi Neema Abdallah, akizungumza kwa niaba ya wenzake, aliwashukuru wanamtandao wa TPF Net Mkoa wa Pwani kwa msaada waliopokea na kuahidi kufanya vizuri kwenye mitihani yao .

Naye Mkuu wa Shule ya Wasichana Mandela, Regina Ngereza, alitoa shukrani kwa Jeshi la Polisi Mkoa wa Pwani kwa ushirikiano waliouonesha tangu kupokea taarifa ya tukio la kuungua kwa bweni hilo, akiwataka waendelee kuwa na moyo huo wa kusaidia jamii.


No comments