WATU 9 WAFARIKI DUNIA, 44 WAJERUHIWA KATIKA AJALI YA BASI NA LORI MOROGORO
Farida Mangube, Morogoro
Watu tisa wamefariki dunia papo hapo na wengine 44 kujeruhiwa baada ya basi la Kampuni ya Hai lenye namba za usajili T523 EKM kugongana na lori lililokuwa limebeba shehena ya sukari lenye namba za usajili T406 CZS – T804 BUB katika eneo la Lugono Melala, barabara kuu ya Morogoro–Iringa.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Alex Mkama, amethibitisha kutokea kwa ajali hiyo, amesema kuwa ilitokea majira ya alasiri ya Juni 12, 2025 katika kijiji cha Lugono Melala.
Kwa mujibu wa Afisa uhisiano Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Morogoro, Scolastica Ndunga hospitali hiyo imepokea miili ya marehemu tisa, ambapo kati ya miili hiyo, mitano ni ya wanaume na minne ni ya wanawake.

Ndunga ameongeza kuwa miili minne kati ya tisa tayari imetambuliwa na ndugu wa marehemu kupitia vitambulisho walivyokuwa navyo. Miili mingine bado haijatambuliwa na imehifadhiwa katika chumba cha kuhifadhia maiti cha hospitali hiyo, ikisubiri utambuzi na taratibu zaidi kutoka kwa familia husika.
Post a Comment