Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi
(INEC) imetoa vibali vya kutoa elimu ya mpiga kura wakati wa uchaguzi mkuu wa
mwaka 2025 kwa taasisi na asasi za kiraia 164 na kibali cha uangalizi wa
uchaguzi kwa taasisi na asasi 76 za ndani ya nchi na 12 za kimataifa.
Taarifa ya Tume kwa vyombo vya
habari iliyotolewa leo Julai 19,2025 na kusainiwa na mkurugenzi wa Uchaguzi wa
INEC, Ndg. Ramadhani Kailima imesema Tume imefikia uamuzi wa kutoa vibali hivyo
katika kikao chake kilichokutana Julai 18, mwaka huu.
“Kwa kuzingatia masharti ya
kifungu cha 10(1) (g) (h) cha Sheria ya Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi Na. 2 ya
mwaka 2024 kikisomwa pamoja na Kanuni ya 22 ya Kanuni za Tume Huru ya Taifa ya
Uchaguzi za mwaka 2024, katika kikao chake maalum kilichofanyika tarehe 18
Julai, 2025 Tume imeridhia na kutoa kibali cha kutoa elimu ya mpiga kura wakati
wa uchaguzi mkuu wa mwaka 2025 kwa taasisi na asasi za kiraia 164.,”alisema taarifa hiyo ya Tume.
Aidha, Kailima amesema katika kikao hicho
imeridhia na kutoa kibali cha uangalizi wa uchaguzi kwa taasisi na asasi 76 za
ndani ya nchi na 12 za kimataifa.
Taarifa hiyo ya Kailima
imesema Tume imefanya uamuzi huo kwa kuzingatia masharti ya kifungu cha
10(1)(i) cha Sheria ya Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi Na. 2 ya mwaka 2024
kikisomwa pamoja na kifungu cha 85(4) cha Sheria ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge
na Madiwani, Na. 1 ya Mwaka 2024 na kanuni ya 13(1) na (2) ya Kanuni za
Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani za Mwaka 2025.
Orodha ya taasisi na asasi
husika inapatikana kupitia tovuti ya Tume ya www.inec.go.tz na mitandao ya kijamii ya Tume Huru ya Taifa ya
Uchaguzi.
“Taasisi na asasi za kiraia
zilizoridhiwa na kupewa kibali cha kutoa elimu ya mpiga kura zitajulishwa kwa
njia ya barua pepe kupitia Mfumo wa Usajili (Accreditation Management System)
ili kujaza taarifa za kuwawezesha kukamilisha taratibu nyingine ikiwemo kuweka
orodha ya watu watakaotoa elimu hiyo,”imesema sehemu ya taarifa hiyo ya Tume.
Aidha, Kwa upande wa taasisi
na asasi za kiraia zilizopata kibali cha kuwa waangalizi wa uchaguzi zimetakiwa
kuwasilisha kwa njia ya Mfumo wa Usajili (Accreditation Management System)
majina ya waangalizi na maeneo waliyopangiwa kufanya uangalizi huo kwa ajili ya
kuwaandalia vibali.
Tume imebainisha kuwa, taarifa
zingine zote muhimu kuhusu utekelezaji wa majukumu ya utoaji wa elimu ya mpiga
kura na uangalizi wa uchaguzi, miongozo na taratibu zote zitatolewa mapema
iwezekanavyo.
Tume imezipongeza taasisi na
asasi za kiraia ambazo zimepata kibali cha kutoa elimu ya mpiga kura na kuwa
waangalizi wa Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani wa Mwaka 2025.

Post a Comment