Header Ads

test

Dkt. Samia: Tumeweka heshima, ujenzi makao makuu Ngome

Rais wa Tanzania, Dkt Samia Suluhu Hassan amesema makao makuu ya ulinzi ni alama ya ukomavu wa kielelezo cha uwezo wa Taifa katika kupanga na kutekeleza miradi mikubwa kwa kutumia fedha za ndani.

Mkuu huyo wa nchi, amesema hatua hiyo ni msingi mzuri wa uhuru wa uamuzi na heshima kwa Tanzania, ikilinganisha na mataifa mengine ya Afrika.
 
Dkt Samia ametoa kauli hiyo leo Jumanne Februari 24,2026 wakati akizindua jengo la makuu mapya ya Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) yaliyopo Kikombo jijini Dodoma yaliyogharimu Sh 121 bilioni.

“Tutakuwa kati ya nchi zilizotoa kipaumbele na heshima kubwa kwa shughuli za ulinzi. Majengo haya yasitupe fahari tu kuwa nayo bali yatumike kuimarisha na kusimamia ulinzi wa Taifa letu,” amesema Dkt Samia.

Na kuongeza kuwa, “majengo haya yatumike kama kituo cha fikra, uchambuzi wa kitaalamu na uratibu wa kisayansi, kwa mikakati na shughuli za ulinzi zinazoendana na wakati tulionao,”

Dkt Samia amefafanua kuwa mazingira ya kiusalama ya kidunia kwa wakati huu, hayalindwi kwa silaha pekee yake bali, nyenzo muhimu ni upatikanaji, uchambuzi na matumizi ya taarifa, teknolojia, mifumo ya mawasiliano na mbinu za kisasa zinazohitaji ubobezi wa kitalaamu na weledi hali ya juu.

Kabla ya Dkt Samia kuzindua jengo hilo, mizinga ilipigwa na Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), huku ndege za kivita zikipita katika anga la eneo yalipojengwa makao makuu hayo kuashiria heshima na umuhimu wa tukio hilo.








No comments