Benki ya Absa Tanzania Yathibitisha Dhamira ya Kuendeleza Uwezeshaji wa Wanawake Kiuchumi kama Nguzo ya Ukuaji wa Taifa
Akizungumza na vyombo vya habari jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi Mtendaji wa Benki hiyo, Obedi Laiser, alieleza kuwa kuwawezesha wanawake ni msingi wa ushindani wa muda mrefu wa uchumi wa Tanzania.
“Uwezeshaji wa wanawake si jambo la hiari katika ukuaji wa uchumi. Ni hitaji la lazima kwa ukuaji,” alisema Bw. Laiser. “Kuwaacha nje karibu nusu ya rasilimali watu wa taifa kushiriki kikamilifu katika uchumi kunasababisha hasara inayoonekana yenye tija.”
Alibainisha kuwa katika Absa, dhana ya ujumuishaji imejengeka ndani ya mfumo wa uendeshaji wa benki hiyo, ikilenga ubunifu wa bidhaa, mifumo ya utoaji mikopo, maendeleo ya uongozi pamoja na ushirikiano wa kimkakati.
“Wanawake daima wameonesha uwezo na uthabiti. Nguvu ilikuwepo siku zote. Kilichokosekana mara nyingi ni fursa, fursa ya kupata mitaji, mitandao na mifumo rasmi,” alisema. “Tunapowawezesha wanawake, hatuchagui tu kundi fulani. Tunachagua mustakabali wa Tanzania.”
Mfano halisi wa dhamira hiyo ni akaunti ya She Business Account, suluhisho maalum lililobuniwa kushughulikia vikwazo vinavyowazuia mara nyingi wanawake wajasiriamali kuingia katika mfumo rasmi wa benki. Bidhaa hiyo inapunguza gharama za uendeshaji wa akaunti huku ikihamasisha ujenzi wa historia ya miamala inayoongeza sifa za kustahili mikopo.
Kutambua kuwa masharti ya dhamana na hali ya kutokuwa rasmi kwa baadhi ya biashara hupunguza upatikanaji wa fedha, benki hiyo pia imeimarisha ushirikiano na taasisi za fedha ndogo. Kupitia mfumo huu wa ufadhili wa ngazi mbalimbali, Absa hutoa mitaji kwa wakopeshaji waliobobea ambao huwafikishia wanawake wajasiriamali katika ngazi za msingi.
Bw. Laiser pia alitofautiana na mtazamo kwamba wanawake ni wakopaji wenye hatari kubwa zaidi. “Dhana kwamba wanawake ni wakopaji hatarishi zaidi haiendani na takwimu za utendaji. Biashara zinazoongozwa na wanawake mara nyingi huonesha nidhamu kubwa ya marejesho ya mikopo na mwenendo endelevu wa kuwekeza tena.”
Mbali na suluhisho za kifedha, Absa inaweka ujumuishaji katika misingi ya taasisi kupitia mipango ya kukuza uongozi. Bw. Laiser ni mdhamini wa programu ya ndani ya ulezi inayojulikana kama “ElevateHer,” inayowawezesha mameneja wanawake wa ngazi ya kati kujenga uwepo wa kiuongozi, kuimarisha ushiriki katika vikao vya bodi, na kuongeza mwonekano wa kimkakati.
Benki hiyo pia huwezesha uhusiano wa ulezi kati ya wakurugenzi wanawake waandamizi na viongozi chipukizi, hatua inayokuza mwendelezo wa uongozi na uhamishaji wa maarifa. Dhamira hii imejikita katika madhumuni ya taasisi ya Absa, ‘Kuiwezesha Afrika ya Kesho Pamoja, hatua moja baada ya nyingine’, na ahadi yake ya chapa, ‘Stori yako ina thamani’.
“Madhumuni yetu yanaakisi imani kwamba ukuaji endelevu hupatikana kwa kufungua uwezo wa mtu mmoja mmoja na wa pamoja. ‘Stori yako ina thamani’ inamaanisha kila mjasiriamali, kila kiongozi na kila ndoto inastahili kutambuliwa, kuungwa mkono na kupewa fursa,” alisema Bw. Laiser.
Aidha, Bw. Laiser alionya kuwa kupunguza kasi ya juhudi za makusudi za uwezeshaji kutaleta gharama zinazoonekana, ikiwemo kudhoofika kwa uthabiti wa kaya, kupungua kwa utofauti wa uongozi na kushuka kwa ushindani wa taifa.
“Katika mazingira ya sasa ya kimataifa, ujumuishaji si suala la pembeni tena. Ni kiini cha uimara wa muda mrefu wa mizania ya kifedha na kasi ya uchumi wa taifa,” alisema.
Kwa Absa Bank Tanzania, uwezeshaji wa wanawake si kampeni ya msimu bali ni uwekezaji wa kimuundo, unaounganisha mafanikio ya kibiashara na maendeleo ya kijamii, na kuiweka benki hiyo kama kichocheo cha mageuzi jumuishi ya uchumi.

Post a Comment