Header Ads

test

Absa Yatajwa Miongoni mwa Chapa 3 Bora za Benki Barani Afrika, Thamani ya Chapa Yavuka R30 Bilioni (TZS Trilioni 4.74), Yashika Nafasi 5 za juu katika Sekta Zote Afrika Kusini.

Johannesburg : Absa Group imetajwa miongoni mwa chapa tatu za benki zenye thamani kubwa zaidi barani Afrika, huku pia ikishika nafasi ndani ya tano bora za chapa zenye thamani kubwa zaidi nchini Afrika Kusini katika sekta zote na makundi yote. 

Hii ni baada ya thamani ya chapa yake kuvuka R30 bilioni (TZS trilioni 4.74) kwa mara ya kwanza. Kwa mujibu wa ripoti inayotolewa na kampuni ya kimataifa ya ushauri wa thamani ya chapa  ‘Brand Finance South Africa 2026’, thamani ya chapa ya Absa imeongezeka hadi kufikia R30.6 bilioni (TZS trilioni 4.83), ikiwa ni ongezeko la asilimia 12 mwaka hadi mwaka, na kuimarisha nafasi ya Kundi hilo kama mtoa huduma za kifedha anayeongoza barani Afrika.

Hatua hii muhimu inaakisi mafanikio ya mkakati wa Absa wa “Stori yako ina Thamani”, uliozinduliwa miaka miwili iliyopita ukiwa na lengo la kumweka mteja katikati ya shughuli za biashara. Mkakati huu, unaozingatia uelewa wa kibinadamu na utoaji wa huduma zilizounganishwa kwa urahisi, umepata mwitikio mkubwa barani Afrika, ukiongeza umuhimu wa chapa, kuimarisha uhusiano na wateja, na kujenga imani imara zaidi.

Katika kipindi cha mwaka uliopita, Absa imeongeza kasi ya ukuaji unaoongozwa na mahitaji ya wateja, kuimarisha uwepo wake barani, na kuharakisha uwezo wake katika masuala ya kidijitali na ubunifu. Uwekezaji unaoendelea katika kuboresha mifumo na kupanua huduma zinazotanguliza matumizi ya kidijitali umeimarisha uwezo wa Kundi kutoa huduma za benki zilizounganishwa na zenye urahisi. Wakati huo huo, Absa imeendelea kuimarisha nafasi yake kama mshirika wa taasisi anayeaminika katika masoko muhimu.

Sydney Mbhele, Afisa Mkuu wa Masoko na Mawasiliano ya Kundi la Absa, alisema; “Kutambuliwa miongoni mwa chapa bora za benki barani Afrika na kushika nafasi ya tano ya juu nchini Afrika Kusini ni uthibitisho mkubwa wa imani ambayo wateja wetu wanaweka kwetu, pamoja na nguvu ya chapa yetu katika soko lenye ushindani mkubwa. Kielezo chetu cha nguvu ya chapa kinaendelea kuonesha uimara na kuboreka, huku viashiria muhimu kama ‘Brand Love’ vikikua kwa kasi. Hii inaonesha uhusiano wa maana tunaoujenga na wateja wetu pamoja na matokeo chanya ya mkakati wetu unaoweka mteja mbele na unaoendeshwa na teknolojia ya kidijitali.

“Miaka miwili iliyopita tulianzisha ‘Stori yako ina Thamani’ kama kauli thabiti ya kumweka mteja katikati ya kila tunachofanya, leo, tunaona ahadi hiyo ikitimia kupitia ushiriki mkubwa zaidi, mahusiano imara, na uzoefu wa chapa ulio karibu zaidi na maisha ya watu katika masoko yetu,” aliongeza.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, chapa imara za benki zina jukumu muhimu katika kujenga imani na uimara wa uchumi wa Afrika Kusini. Absa inaendelea kujitolea kutekeleza jukumu hili kwa kuzingatia utoaji wa suluhisho zilizounganishwa na zinazotanguliza huduma za kidijitali ili kusaidia wateja, taasisi na jamii kukabiliana na mazingira yanayobadilika kwa kasi.

Utendaji huu mzuri wa chapa unaungwa mkono na matokeo imara ya kifedha. Absa Group iliripoti ongezeko la asilimia 12 la faida kuu hadi kufikia R24.8 bilioni, likichangiwa na faida kubwa kabla ya makadirio ya hasara na kupungua kwa mikopo chechefu, hali inayoonesha utekelezaji makini na mfumo thabiti wa uendeshaji.

Kundi pia lilirekodi ongezeko kubwa la matumizi ya huduma za kidijitali, ambapo idadi ya wateja wanaotumia huduma hizo iliongezeka kwa asilimia 11 na kufikia milioni 3.6 katika mwaka wa fedha 2025. Hii inaashiria mwelekeo unaoendelea wa matumizi ya huduma rahisi za benki kupitia programu za simu ya mkononi. 

Ukuaji huu umechangiwa na ongezeko la watumiaji wa Absa Banking App, ambapo watumiaji hai katika sekta ya benki kwa wateja binafsi na wateja maalumu waliongezeka kwa asilimia 14 hadi kufikia milioni 2.9. Upakuaji mpya wa programu uliongezeka kwa asilimia 94, ukichangiwa na maboresho endelevu, utendaji bora zaidi, na uzoefu rahisi kwa mtumiaji.

Absa inatoa shukrani zake kwa wafanyakazi wake, wateja na wadau wote ambao mchango wao umewezesha kufikiwa kwa mafanikio haya muhimu.

“Kuvuka hatua hii si tu kielelezo cha tulipo leo, bali ni ishara ya mwelekeo wetu wa baadaye,” alihitimisha Mbhele. “Dhamira yetu ya ‘Kuiwezesha Afrika ya Kesho Pamoja’ inaonesha kujitolea kwa kina kushirikiana na watu na jamii tunazozihudumia katika kujenga maendeleo. Kila ubunifu, kila ushirikiano na kila mawasiliano na mteja ni sehemu ya simulizi kubwa zaidi, ambapo tunajenga mustakabali jumuishi, imara na wenye fursa nyingi kwa bara la Afrika, hatua moja baada ya nyingine.”


No comments