Header Ads

test

MWANG’ONDA AZINDUA MRADI WA USAFIRISHAJI WA VIJANA MKURANGA

 



KIONGOZI wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa 2026, Wazo Mwang’onda, amezindua mradi wa basi dogo wa kikundi cha vijana cha UNAMA, kinachotoa huduma ya usafirishaji wa abiria katika kijiji cha Picha ya Ndege, kata ya Vikindu wilayani Mkuranga mkoani Pwani, Akizungumza wakati wa uzinduzi huo Aprili 24, 2026, Mwang’onda amewapongeza vijana hao kurejesha fedha za mkopo na kuaminiwa kuongezewa fedha kiasi cha milioni 85.2, kupitia asilimia 10 ya mapato ya ndani ya halmashauri. 


Aidha amewahimiza vijana kote nchini kutumia kikamilifu fursa ya mikopo ya asilimia 10 inayotolewa na halmashauri, akieleza kuwa ni nyenzo muhimu ya kujikwamua kiuchumi na kujenga ajira binafsi.
Mbunge wa Jimbo la Mkuranga, Abdallah Ulega, ameeleza utekelezaji wa mikopo hiyo unatoa fursa halisi kwa vijana kujiajiri kupitia miradi yenye tija.

“Tunampongeza Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa maelekezo ya utoaji wa mikopo kupitia halmashauri, pamoja na kusisitiza ukusanyaji wa mapato ya ndani unaowezesha kutengwa kwa asilimia 10 kwa ajili ya vijana, wanawake na watu wenye ulemavu,” amesema Ulega.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Mkuranga, Khadija Nasir, amesema jumla ya miradi nane yenye thamani ya shilingi milioni 39.5 imepitiwa na Mwenge wa Uhuru mwaka 2026, baada ya kupokelewa kutoka Wilaya ya Kisarawe.

Kati ya Miradi hiyo ni usambazaji wa nishati safi ya kupikia, kiwanda cha vinywaji baridi cha Yaket International, ujenzi wa uzio wa Shule ya Sekondari Mwinyi, ujenzi wa boksi kalavati, pamoja na mradi wa maji katika kijiji cha Sotele.

Mwenge wa Uhuru umefikisha siku ya saba mkoani Pwani tangu ulipopokelewa Aprili 18, 2026, na unatarajiwa kuendelea na mbio zake Aprili 25, 2026 katika Wilaya ya Kibiti.




No comments