TMDA YAUNGANISHA TANCIS NA RIMS, SASA WAINGIZAJI WA MIZIGO MIKUBWA YA FORODHA KUTUMIA MFUMO WA TANCIS
MAMLAKA ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA) imewatangazia waingizaji wa mizigo mikubwa ya forodha ya bidhaa za Dawa, Vifaa Tiba na Vitendanishi nchini, kuwa mifumo ya TANCIS-TRA na RIMS-TMDA imeunganishwa ili kuongeza ufanisi katika kuingiza na kutoa shehena za bidhaa hizo nchini kwa njia ya kielektroniki.
Kwa mujibu wa taarifa kwa Umma iliyotolewa na Mkurugenzi Mkuu wa TMDA, Dk. Adam Fimbo ameeleza kuwa, Lengo kuu la muunganiko huo ni kurahisisha michakato ya uombaji vibali kuwa na sehemu moja ya kuingiza taarifa, pamoja na kuboresha ufuatiliaji na shughuli za udhibiti wa maombi ya kuingiza na kutoa bidhaa nchini.
"Mnajulishwa rasmi kuwa kuanzia tarehe 1 Mei, 2026 maombi yote yaliyokuwa yanapitia TMDA-RIMS na TRA-Forodha kwa ajili ya kutolea taarifa (declaration) yatafanyika moja kwa moja katika mfumo wa TANCIS.
Ili kuepusha Hoja zisizo za lazima na kurahisisha huduma za upatikanaji wa vibali, mnakumbushwa kuzingatia; Usahihi wa taarifa za bidhaa zinazosimamiwa na TMDA (ikijuimuisha namba za usajili za bidhaa na majengo); na Wadau wote watatakiwa kushirikiana na Wakala wa Forodha kwa ukaribu ili kuthibitisha usahihi wa taarifa za kitaalam na nyaraka hitajika." Imeeleza taarifa hiyo kwa Umma.
Aidha, TMDA imewataka kuzingatia kuwa, tangazo hilo linawahusu waingizaji wa mizigo mikubwa ya forodha, na si waingizaji kwa matumizi binafsi (personal use).
Post a Comment