Absa Yaona Msimamo wa Uchumi wa Dunia Kuipa Tanzania Fursa ya Ushindani wa Kibiashara
Benki ya Absa Tanzania, imeeleza kuwa changamoto na misukosuko ya uchumi wa dunia zinaweza kuwa fursa muhimu kwa Tanzania kujijengea ushindani wa kiuchumi na biashara katika soko la kimataifa.
Kauli hiyo ilitolewa jijini Dar es Salaam leo katika hafla iliyoandaliwa na benki hiyo kwa viongozi waandamizi wa sekta za kibiashara ikilenga kujadili namna biashara za Tanzania zinavyoweza kubadili hali ya sintofahamu ya uchumi wa dunia kuwa fursa za kimkakati.
Mkutano huo uliwakutanisha wataalamu wa uchumi wa jumla kutoka Absa Group nchini Afrika Kusini
pamoja na wataalamu wa ndani, ambao walijadili mwenendo wa uchumi wa dunia na kutoa mbinu za kusaidia biashara kukabiliana na changamoto zinazotokana na siasa za kimataifa, mfumuko wa bei, mabadiliko ya tabianchi na kuyumba kwa masoko ya fedha.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa kikao hicho, Mkurugenzi wa Kitengo cha Mashirika Makubwa wa Benki ya Absa Tanzania, Bi. Nellyana Mmanyi, alisema kutokuwa na uhakika katika uchumi wa dunia sasa si jambo la muda mfupi bali ni hali ya kudumu inayohitaji biashara kuwa na uwezo wa kujipanga kimkakati.
Alisema mafanikio ya biashara katika mazingira ya sasa yatategemea uwezo wa taasisi kubadili changamoto kuwa fursa za ushindani.
“Misukosuko ya kiuchumi duniani si hali ya mpito tena, bali ni uhalisia wa kudumu. Kwa Tanzania, huu ni wakati wa kuhitaji uongozi wenye taarifa sahihi, wepesi wa kufanya maamuzi ya kimkakati, na ushirikiano unaounganisha uzoefu wa kimataifa na utekelezaji wa ndani,” alisema Bi. Nellyana.
Katika kikao hicho, timu ya watafiti wa uchumi kutoka Absa Group iliwasilisha tathmini ya hali ya uchumi wa dunia na Afrika, ikieleza namna mvutano wa kisiasa duniani unavyoathiri masoko ya nishati, kuongeza mfumuko wa bei, pamoja na changamoto za viwango vya riba na athari zake kwa uhimilivu wa madeni.
Majadiliano pia yaligusia athari za mabadiliko ya tabianchi katika usalama wa chakula na uthabiti wa kijamii, huku ikielezwa kuwa utegemezi mkubwa wa Afrika kwa bidhaa za nje na mazingira ya kifedha ya kimataifa unaongeza shinikizo kwa uchumi wa bara hilo.
Hata hivyo, wataalamu hao walieleza kuwa Tanzania inaendelea kuonesha uimara wa kiuchumi kutokana na mazingira tulivu ya sera za fedha, ukuaji mzuri wa pato la taifa ukilinganishwa na nchi nyingine za ukanda huo, pamoja na nafasi yake ya kimkakati katika mabadiliko ya biashara na nishati duniani.
Aidha Bi. Nellyana alisema Tanzania ina msingi imara wa kiuchumi ambao unaweza kusaidia nchi kunufaika na mabadiliko ya sasa ya uchumi wa dunia kupitia uwekezaji, biashara na ukuaji wa muda mrefu.
Pamoja na hayo, wataalamu wa Trade Finance na Global Markets wa Absa waliwasilisha mbinu mbalimbali za kusaidia biashara kujikinga dhidi ya hatari za kiuchumi, ikiwemo suluhisho za mtaji wa biashara, ulinzi wa minyororo ya usambazaji, pamoja na matumizi ya mifumo ya kudhibiti hatari za ubadilishaji wa fedha za kigeni, viwango vya riba na masoko ya fedha.
Kwa upande wake, Mchumi Mwandamizi katika masuala ya Uchumi wa Absa Group, Bw. Phumelele Mbiyo, alisema utekelezaji wa mikakati ndiyo jambo muhimu zaidi katika mazingira ya sasa ya uchumi wa dunia.
Alisema Absa inaendelea kushirikiana na wateja wake si tu kwa kutoa huduma za kifedha, bali pia kwa kuwapatia utaalamu, taarifa na mifumo ya kufanya maamuzi sahihi hata katika mazingira yenye sintofahamu kubwa.
Kupitia kikao hicho, Absa ilisisitiza dhamira yake ya “Kuiwezesha Afrika ya kesho, pamoja… hatua moja baada ya nyingine,” ikiwa ni sehemu ya juhudi za benki hiyo kusaidia biashara za Tanzania kupitia tafiti za kiuchumi, utaalamu wa kitaalamu na ushirikiano wa muda mrefu.
Post a Comment