POLISI PWANI YACHUNGUZA UTATA KUBADILISHWA KICHANGA HOSPITAL BAGAMOYO
Mwamvua Mwinyi, Bagamoyo Juni 7,2026
JESHI la Polisi Mkoa wa Pwani limeanza uchunguzi wa kina kufuatia malalamiko ya mwanamke mmoja mkazi wa Gongo la Mboto, Dar es Salaam, anayodai kubadilishiwa mtoto baada ya kujifungua kwa njia ya upasuaji katika Hospitali ya Wilaya ya Bagamoyo.Akitoa ufafanuzi kuhusu tukio hilo, kamanda wa Polisi mkoani Pwani,Salim Morcase alimtaja mlalamikaji huyo kuwa ni Filomena Richard Mataris (36), ambaye pamoja na mume wake, Carlos Kapata, walifika Kituo cha Polisi Bagamoyo Juni 5, 2026 na kutoa taarifa ya madai hayo.
Kwa mujibu wa Morcase, Filomena alihamia Kerege wilayani Bagamoyo Aprili 14, 2026 kwa ndugu yake Avetha Mabadiliko kwa ajili ya kupata uangalizi wa karibu wakati wa ujauzito.
"Mei 17, 2026 alipata uchungu wa kujifungua na kupelekwa Hospitali ya Kerege, ambapo baada ya kufanyiwa uchunguzi alibainika kuwa na dalili za uzazi pingamizi na kuhamishiwa Hospitali ya Wilaya ya Bagamoyo kwa ajili ya upasuaji."
" Mei 18, 2026 majira ya saa 8:30 usiku, Filomena alijifungua mtoto wa kiume kwa njia ya upasuaji na kudai kuwa alimwona na kumbeba mtoto huyo akiwa mzima wa afya, baada ya kuhamishiwa wodini, alidai kuoneshwa picha ya mtoto kupitia simu ya daktari na kuambiwa kuwa ndiye mtoto wake aliyefariki dunia.
Mama huyo alifafanua kuwa mtoto aliyeoneshwa kwenye picha alikuwa na changamoto mbalimbali za kiafya ikiwemo kichwa kilichobonyea na uvimbe kifuani, hali ambayo alisema ilikuwa tofauti na mtoto aliyemuona mara baada ya kujifungua.
Aidha, Filomena alidai kuwa aliambiwa mwili wa mtoto huyo ulikwishakabidhiwa kwa ndugu zake kwa ajili ya mazishi, bila yeye wala baba wa mtoto kushirikishwa au kufahamishwa kuhusu taratibu hizo.
Katika hatua za awali za uchunguzi, Kaimu Mganga Mkuu wa Hospitali ya Wilaya ya Bagamoyo, Dk. Mariam Ngwele, alieleza kuwa mtoto aliyezaliwa alikuwa na matatizo ya kiafya ikiwemo kichwa kilichobonyea, uvimbe kifuani na changamoto za upumuaji.
Dk. Ngwele, anasema mtoto huyo alifariki muda mfupi baada ya kuzaliwa licha ya jitihada za kitabibu zilizofanyika.
Post a Comment