Header Ads

test

RIDHIWANI: UTUMISHI WA UMMA UENDANE NA KASI YA TEKNOLOJIA

Ahimiza matumizi AI kurahisisha utoaji huduma za umma

Na. Jawadu Kinyobwa – Dar es salaam

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. Ridhiwani Jakaya Kikwete (Mb), amesema utumishi wa umma unapaswa kuendana na kasi ya maendeleo ya teknolojia ili kuongeza ufanisi katika utoaji wa huduma na kufanikisha utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 kwa pande zote za Muungano.

Mhe. Kikwete amesema hayo Junin17, 2026 katika Kongamano la Pili la Utumishi wa Umma Tanzania 2026 lililofanyika katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNCC) jijini Dar es Salaam, ambalo limewakutanisha wadau mbalimbali kujadili nafasi ya utumishi wa umma katika kufanikisha utekelezaji wa Dira ya Taifa 2050.

Amesema utekelezaji wa Dira ya Taifa 2050 unahitaji utumishi wa umma wenye uwajibikaji, ufanisi, ubunifu na uwezo wa kusimamia kwa mafanikio sera na mipango ya Serikali ili kutoa huduma bora kwa wananchi na kujenga imani kwa Serikali yao.

“Dira ya Taifa 2050 kwa Tanzania Bara na Zanzibar zimeweka msingi wa kujenga taifa lenye uchumi imara, linalotumia maarifa, ubunifu na teknolojia katika kuleta maendeleo endelevu. Mafanikio ya utekelezaji wake yanategemea kwa kiasi kikubwa uwepo wa utumishi wa umma wa kisasa na wenye tija,” amesema Mhe. Kikwete.

Aidha, amesisitiza umuhimu wa matumizi ya teknolojia za kisasa ikiwemo Akili Bandia (AI) katika kurahisisha utoaji wa huduma za umma, kupunguza urasimu, kuongeza uwazi na kuimarisha uwajibikaji kwa wananchi.

Ameeleza kuwa pamoja na matumizi ya teknolojia, utumishi wa umma unatakiwa kuimarisha ushirikiano kati ya Serikali, sekta binafsi na wadau wa maendeleo ili kuchochea ukuaji wa uchumi na kuharakisha utekelezaji wa vipaumbele vya maendeleo ya taifa.

Mhe. Kikwete pia amekitaka Chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania (TPSC) na Chuo cha Utawala wa Umma Zanzibar (IPA) kuendelea kutekeleza majukumu yake ya msingi ya kutoa mafunzo, kufanya tafiti tumizi na kutoa ushauri wa kitaalamu ili kuzalisha watumishi wenye uwezo wa kukabiliana na mahitaji ya sasa na ya baadaye ya utumishi wa umma.
Awali akizungumza Mkuu wa Chuo na Mtendaji Mkuu Dkt. Ernest Mabonesho, amesema kongamano hilo limeandaliwa kama jukwaa la kuwakutanisha wadau mbalimbali kwa lengo la kujadiliana na kubadilishana uzoefu kuhusu namna bora ya kuimarisha utendaji wa taasisi za umma katika mazingira yanayobadilika kwa kasi. 



















No comments