OCPD yawanoa Waandishi wa Sheria kukabili mahitaji ya Taifa.
Na: Calvin Gwabara – Dodoma.
Ofisi ya Mwandishi Mkuu wa Sheria
(OCPD) imeendelea kuwekeza katika kuwaendeleza watumishi wake kitaaluma kwa
kuwapatia fursa za mafunzo ndani na nje ya nchi, hatua inayolenga kuongeza
idadi ya wataalamu wenye weledi, utaalamu wa kisekta na uwezo wa kuandaa sheria
bora zinazowezesha utekelezaji wa sera na mipango ya Serikali.
![]() |
| Mwandishi Mkuu wa Sheria (CPD) Bwana Onorius John Njole wakati akiongea na Mwandishi wetu kuhusu mpango huo wa mafunzo. |
Hayo yamebainishwa na Mwandishi
Mkuu wa Sheria (CPD) Bwana Onorius John Njole wakati akiongea na Mwandishi wetu
kuhusu jitihada zinazochukuliwa na ofisi yake katika kuiwezesha nchi kupata
sheria bora zinazokwenda na wakati.
Bwana Njole amesema Uandishi wa Sheria
ni taaluma maalumu yenye misingi, kanuni na viwango vyake, hivyo inahitaji
mafunzo mahsusi na uwekezaji endelevu katika kujenga uwezo wa wataalamu.
“Ingawa Waandishi wa Sheria ni
Wanasheria, si kila Mwanasheria ni Mwandishi wa Sheria mtu anakuwa Mwandishi wa
Sheria baada ya kupata taaluma maalumu ya uandishi wa Sheria,” amesema Njole.
Amesema mkakati wa Ofisi hiyo
haujajikita katika kuwafundisha waandishi namna ya kuandika sheria pekee bali
pia kuwajengea utaalamu katika sekta ambazo sheria wanazoandika zinalenga
kuzisimamia kwa kuwa uelewa huo huwasaidia kutambua mahitaji halisi ya sekta na
kuandaa sheria zinazoweza kutatua changamoto na kuwezesha utekelezaji wa
mipango ya Taifa.
Mwandishi huyo Mkuu wa Sheria
amesema kwa kutambua umuhimu wa taaluma hiyo, Ofisi ya Mwadishi Mkuu wa Sheria
(OCPD) imekuwa ikiwapeleka watumishi kupata mafunzo katika vyuo na taasisi
mbalimbali ndani na nje ya nchi zilizobobea, huku baadhi wakipata utaalamu
katika maeneo mahsusi kama Kodi, Sheria za Bahari na Uandishi wa Sheria.
Aidha amesema kuwa OCPD pia
imeweka mkazo katika mafunzo ya ndani kwa kuwa sehemu kubwa ya uandishi wa
sheria hujifunzwa kupitia utekelezaji wa majukumu ya kila siku. Ofisi hiyo
imekuwa na mfumo wa kufundishana baina ya waandishi wa sheria, ikiwemo madarasa
ya maeneo mbalimbali ya uandishi wa sheria yanayofanyika kila Jumatatu.
“Katika mwaka uliomalizika, Waandishi
wawili walipelekwa Chuo cha West Indies, wengine tisa Chuo cha Sheria cha
Zambia kwa ajili ya mafunzo ya uandishi wa sheria, huku mpango wa mwaka 2026
ukilenga kupeleka waandishi wengine wawili Zambia na wawili katika Chuo cha
Sheria cha London” alieleza Njole.
Aliongeza “Uwekezaji huu pia
unalenga kuwa na wataalamu wenye utaalamu wa kisekta, ambapo katika mwaka
uliomalizika waandishi wawili walipata shahada za uzamili katika eneo la kodi,
huku waandishi wanne wakipata shahada za uzamili katika Sheria za Bahari nchini
Malta”.
Mwandishi huyo Mkuu wa Sheria alisema
lengo la muda mrefu ni kuhakikisha Tanzania inakuwa na wataalamu wa kutosha
katika uandishi wa sheria wenye uwezo wa kukidhi mahitaji ya ndani na pia kutoa
huduma za uandishi wa sheria katika nchi nyingine, hususan ndani ya Jumuiya ya
Madola.
Miongoni mwa wanufaika wa mpango
huo ni Boniphas Mondu Giabe aliyepata
fursa ya kusoma Shahada ya Uzamili katika Uandishi wa Sheria katika Chuo Kikuu
cha West Indies, Kampasi ya Cave Hill, nchini Barbados ambaye amesema mafunzo
hayo yamemsaidia kuongeza ujuzi katika Uandishi wa Sheria na kumjengea uelewa
wa umuhimu wa kuandaa sheria kwa lugha inayoeleweka kwa urahisi na
inayozingatia misingi ya kikatiba na haki za binadamu.
“Moja ya mambo muhimu
niliyojifunza ni kwamba sheria zinapaswa kuandikwa kwa lugha na mtindo
unaowawezesha watumiaji kuzielewa kwa urahisi lakini pia zinapaswa kuzingatia
misingi ya kikatiba pamoja na haki za binadamu,” amesema Giabe.
Amesema maarifa aliyoyapata
katika maeneo ya sheria za utawala, sheria za katiba, mafuta na gesi
yanaendelea kumsaidia katika utekelezaji wa majukumu yake, huku akishirikisha
ujuzi huo na waandishi wengine wa sheria katika kuandaa sheria bora na
zinazotabirika.
Nae mnufaika mwingine Bi. Loveness Jacob aliyepata ufadhili wa
Shahada ya Uzamili katika Sheria za Kimataifa za Baharini kutoka Chuo cha
Kimataifa cha Sheria za Baharini (IMO International Maritime Law Institute –
IMLI), nchini Malta, ambapo amesema mafunzo hayo yamemwongezea utaalamu katika
eneo muhimu la kimkakati kwa Serikali na Ofisi ya Mwandishi Mkuu wa Sheria.
“Utaalamu nilioupata utasaidia
katika uandaaji wa Sheria zinazotokana na mikataba ya kimataifa ya baharini,
uandaaji wa nyaraka za utekelezaji wa mikataba hiyo na kuimarisha usimamizi wa
masuala ya bahari na kuchangia katika kukuza uchumi wa buluu kupitia uandishi
wa sheria za sekta hiyo, alisema Jacob.
Amesema mafunzo hayo pia yamempa
fursa ya kupata uzoefu wa vitendo katika masuala ya sheria za kimataifa kupitia
ushiriki katika mkutano wa Kamati ya Kisheria ya Shirika la Kimataifa la Bahari
(IMO Legal Committee) ambapo alijifunza namna nchi zinavyoshiriki katika
mijadala ya kimataifa na kuwasilisha hoja za kisheria.
Aidha kwa upande wake Bi. Winfrida Mwera ambaye ni Kaimu Mkurugenzi
Msaidizi wa Uandishi na Ufasiri wa Sheria Ndogo katika OCPD, aliyepata fursa ya
kusoma Postgraduate Diploma in Legislative Drafting, kwa lengo la kuimarisha
uwezo wake katika kuandaa na kurekebisha miswada ya sheria, amesema mafunzo
hayo yamemwongezea ujuzi katika matumizi ya mbinu na misingi mbalimbali ya
uandishi wa sheria, pamoja na uwezo wa kuandaa sheria zilizo wazi, sahihi na
zenye ufanisi.
“Nitatumia ujuzi na maarifa
niliyoyapata kupitia mafunzo haya katika kuandaa rasimu za sheria zenye ubora
wa juu, kupunguza mapungufu katika uandishi wa sheria na kutoa mchango wenye
tija katika utekelezaji wa majukumu ya kila siku ya OCPD,” amesema Mwera.
Amesema uwekezaji huo umechangia
kuongeza uwezo wa watumishi na kuboresha utendaji wa taasisi huku akitoa wito
wa kuendelea kutolewa kwa fursa za mafunzo kwa wataalamu wengine.
Katika kuhakikisha mafunzo
wanayoyapata kutoka ndani na nje ya nchi Ofisi hiyo ina siku maalumu kila wiki
kwa wahitimu kukutana na watumishi wenzao na kuwafndisha na kujengeana uwezo
kupitia mafunzo ya ndani ili wote wanufaike na kuchangia ubora wa kazi za ofisi
kwa maslahi mapana ya Taifa.

%20%20Bwana%20Onorious%20John%20Njole.jpg)

Post a Comment