Header Ads

test

RC MANYARA AISHAURI TMDA KUIMARISHA UTOAJI ELIMU KWA WANANCHI KUHUSU MATUMIZI SAHIHI DAWA,VIFAA TIBA

 NA EMMANUEL  MASSAKA 

 
MAMLAKA ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA) imeshauriwa kuendelea kuimarisha utoaji wa elimu kwa wananchi kuhusu matumizi sahihi ya dawa na vifaa tiba.Ushauri huo umetolewa na Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Bi. Queen Sendiga alipokuwa akifungua kikao cha siku mbili kati ya TMDA, wahariri na waandishi wa habari kutoka mikoa ya Manyara, Arusha na Kilimanjaro, kilichofanyika mkoani Manyara.


Lengo la kikao hicho ni kwa kuwajengea uelewa kuhusu majukumu ya TMDA, udhibiti wa dawa, vifaa tiba na vitendanishi pamoja na changamoto zinazojitokeza katika eneo hilo.

Ametumia nafasi hiyo kueleza kuwa taarifa sahihi kuhusu bidhaa za tiba ni muhimu kwa sababu sekta hiyo inahusisha moja kwa moja afya na mustakabali wa jamii, hivyo wananchi wanapaswa kupata taarifa sahihi na kwa wakati ili waweze kufanya maamuzi salama.

Mkuu wa Mkoa huyo amesema wanapozungumzia bidhaa za tiba wanazungumzia afya na mustakabali wa jamii yetu kwa ujumla. Hivyo ni muhimu wananchi wapate taarifa sahihi kuhusu dawa na vifaa tiba.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Dawa za Binadamu na Mifugo wa TMDA, Dkt. Yona Mwalwisi, amesema mamlaka hiyo inaendelea kutekeleza majukumu yake kwa mujibu wa Sheria ya Dawa na Vifaa Tiba, Sura ya 219, inayoiwezesha kusimamia ubora, usalama na ufanisi wa dawa, vifaa tiba na vitendanishi nchini.

“TMDA imejenga utamaduni wa kukutana na wahariri na waandishi wa habari kila mwaka katika maeneo mbalimbali nchini ili kujadili mafanikio, changamoto na mikakati ya pamoja ya kuboresha udhibiti wa bidhaa za tiba na kuongeza uelewa wa wananchi kuhusu huduma zinazotolewa na mamlaka hiyo.”

Ameongeza utafiti wa kuridhika kwa wananchi na wateja uliofanywa na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, hususan Shule ya Biashara Desemba 2022 katika halmashauri 35 za mikoa 16, umeonesha kuongezeka kwa uelewa kuhusu TMDA kutoka asilimia 47 mwaka 2020, huku kiwango cha kuridhika na huduma za mamlaka hiyo kikiwa asilimia 82.

“Mafanikio hayo yamechangiwa kwa kiasi kikubwa na ushirikiano kati ya TMDA na vyombo vya habari, ambavyo vimekuwa daraja muhimu la kufikisha elimu kwa wananchi kuhusu matumizi sahihi ya dawa na vifaa tiba, pamoja na kuwaelimisha kuhusu hatari za bidhaa bandia, duni na zisizosajiliwa.”

Aidha, amesema TMDA imeendelea kushikilia cheti cha mfumo wa usimamizi wa ubora ISO 9001:2015 pamoja na ithibati ya maabara kwa kiwango cha ISO 17025:2017, jambo linalothibitisha kuwa mifumo na huduma zinazotolewa na mamlaka hiyo zinakidhi viwango vya kimataifa.

Amesema TMDA pia imetambuliwa na Shirika la Afya Duniani (WHO) kuwa mamlaka iliyofikia ngazi ya tatu ya ukomavu wa mifumo ya udhibiti wa bidhaa za tiba, huku ikiendelea na juhudi za kufikia ngazi ya nne, ambayo ndiyo ya juu zaidi, na kuendelea kuwa miongoni mwa mamlaka zinazoongoza barani Afrika.

Pamoja na hayo ameeleza mamlaka hiyo imeimarisha ufuatiliaji wa usalama wa dawa na chanjo baada ya kuingia sokoni, ikiwa ni pamoja na kuongeza vituo vya kufuatilia madhara ya dawa na chanjo hadi kufikia vituo 33 nchini.

Aiidha mtandao wa maabara hamishika ukiongezeka kutoka 19 hadi 28, hatua inayowezesha upimaji wa sampuli katika maeneo mbalimbali kwa wakati. TMDA pia imeweka vituo vya maabara katika vituo vyote 16 rasmi vya forodha vinavyoingiza bidhaa za tiba nchini.


























No comments