WANAFUNZI CHALINZE MODERN ISLAMIC WAFANYA UPASUAJI, ICT NA KUTENGENEZA MASHINE YA SABUNI YA MAJI
Na Mwamvua Mwinyi, Chalinze. Agosti 13, 2026
Shule ya Chalinze Modern Islamic ,Mkoani Pwani, inawajengea wanafunzi ujuzi wa vitendo katika fani mbalimbali ikiwemo udaktari, teknolojia ya habari na mawasiliano (ICT), zimamoto pamoja na utengenezaji wa sabuni za maji, ikiwa ni sehemu ya kuwaandaa kujiajiri na kutumia vipaji baada ya masomo.
Akizungumza na waandishi wa habari kuhusu maendeleo ya shule hiyo, Mwalimu Mkuu Msaidizi, Rashid Stambuli, alisema mpango huo unalenga kuwapa wanafunzi uelewa mpana wa taaluma wanazozisoma, huku wakitumia vipaji vyao kuwa msaada kwa familia na jamii.
Alieleza shule hiyo imekuwa ikitekeleza mtaala kwa kuunganisha masomo ya darasani na vitendo, kwa kuwa wanafunzi wanahitaji kuona na kufanya kile wanachojifunza ili kuongeza uelewa na kuwajengea hamasa ya kusomea taaluma mbalimbali.
“Ni kawaida yetu kufuata mitaala na maagizo yanayotolewa na serikali, mitaala inabadilika na kuboreshwa ambapo watoto wasiwe darasani pekee, bali wanapaswa kutoka kuona na kuamini kwa vitendo,” alifafanua Stambuli.
Alibainisha kuwa, tofauti na baadhi ya shule zinazowapeleka wanafunzi kujifunza kwenye mbuga za wanyama ama maabara, Chalinze Islamic Modern School imeongeza mazingira ya kujifunzia ndani ya shule kwa kuwafundisha wanafunzi kwa kutumia wanyama kama sungura katika kujifunza masuala ya sayansi na udaktari.
“ Tunawaleta wanyama kama sungura shuleni na kuangalia mfumo wa chakula tumboni, Hatuishii hapo, wanafunzi wanaonyeshwa namna ya kufanya huduma mbalimbali za kitabibu kama kuweka drip ,kufunga ogo na matumizi ya oksijeni,” alisisitiza Stambuli.
Stambuli alisema mpango huo umeanza kuzaa matunda, akieleza kuwa baadhi ya wanafunzi wa kike wameanza kuonyesha umahiri katika masuala ya udaktari tangu wakiwa darasa la sita na sasa wamefikia kidato cha pili.
Alitoa wito kwa wazazi na walezi kutowapangia watoto masomo au taaluma bila kuzingatia vipaji na uwezo wao, akisema malezi yanapaswa pia kuwapa nafasi watoto kukuza vipaji walivyonavyo.
Katika eneo la kukabiliana na majanga ya moto, Stambuli alieleza, shule hiyo ilianza kushirikiana na Jeshi la Zimamoto na Uokoaji kutoa mafunzo kwa wanafunzi na wafanyakazi takribani miaka mitatu iliyopita.
Alisema mafunzo hayo yalionekana kuwa muhimu zaidi baada ya kutokea kwa janga la moto shuleni wiki mbili baada ya kuanza kwa utaratibu huo, ambapo baadhi ya wafanyakazi na wanafunzi waliokuwa wamepata mafunzo waliweza kushiriki katika hatua za awali za kukabiliana na tukio hilo.
“Hii ni taasisi ambayo ina watu zaidi ya 1,000 katika kituo na tunatumia majiko pamoja na umeme, hivyo tahadhari na elimu ya kukabiliana na majanga ya moto ni lazima na elimu hiyo ni endelevu,” anasisitiza Stambuli.
Kwa upande wake, Mkaguzi Msaidizi wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji ambaye pia ni Mkuu wa Kituo cha Zimamoto Chalinze, Mariah Gulam Kasekwa, anasema mkakati wa jeshi hilo ni kuhakikisha jamii inapata elimu ya kujikinga na majanga ya moto, ikiwemo kutambua vyanzo vya moto na hatua za kuchukua pindi moto unapotokea.
Kasekwa alisema elimu hiyo ni muhimu zaidi katika maeneo yenye mikusanyiko mikubwa ya watu kama shule, kutokana na uwepo wa wanafunzi na matumizi ya nishati mbalimbali.
Akizungumza kuhusu ndoto yake, mwanafunzi wa kidato cha pili wa Chalinze Islamic Modern School, Shadya Maulid, alisema analenga kuwa daktari na tayari amekuwa akitumia ujuzi anaoupata shuleni kuwasaidia wanafunzi wenzake kujifunza masuala ya afya.
“Kwa sasa nafundisha wanafunzi wenzangu wa shule ya msingi akiwemo Haitham Swedi, Aisha Adam, Rahma Ally na Baraka Sharifu. Tunatumia zaidi kufanya vitendo kupitia sungura ambao wanafugwa hapa shuleni,” alieleza Shadya.
Naye mwanafunzi wa darasa la saba, Baraka Sharifu, ambaye amebobea katika mafunzo ya awali ya zimamoto na baadhi ya vitendo vya huduma za afya ikiwemo uwekaji wa drip, aliishukuru serikali kwa kuboresha mitaala na kusaidia upatikanaji wa vifaa vya kufundishia vinavyowawezesha wanafunzi kujifunza kwa vitendo.
Alielezea kwamba, mafunzo hayo yamewajengea wanafunzi ujasiri, uelewa na hamasa ya kuendeleza vipaji vyao katika taaluma mbalimbali.

.jpeg)


Post a Comment