OFISI YA WAKILI MKUU WA SERIKALI WALINZI WA UCHUMI WA TAIFA
Katibu Mkuu wa Wizara ya Katiba na Sheria, Dkt. Seif Shekalaghe ameipongeza Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali (OWMS) kwa utekelezaji wa majukumu ya kuendesha mashauri ya madai na usuluhishi kwa niaba ya Serikali na taasisi ndani na nje ya nchi kwa ufanisi. Hii imedhihirisha kuwa OWMS inatekeleza majukumu hayo nyeti ya kulinda maslahi mapana ya taifa la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Hayo yamesemwa na Dkt. Shekalaghe wakati wa kikao kazi chake na viongozi na wajumbe wa menejimenti ya OWMS kilichofanyika jijini Dar es Salaam.
“Nimebaini na kutambua kuwa OWMS ni walinzi wa uchumi wa taifa kwa kuwa mmeendesha na kushinda mashauri ya madai na usuluhishi. Naelewa umuhimu wa OWMS katika kulinda uchumi wa nchi kwa uzalendo mkubwa. Wizara ina dhamana ya kuhakikisha kuwa OWMS inawezeshwa ili ifanye kazi zake vizuri zaidi.
Wakili Mkuu wa Serikali, Dkt. Ally Possi alisema kuwa OWMS kwa takribani kipindi cha miaka nane imeendesha na kushinda mashauri ya usuluhishi na madai ndani na nje ya nchi kwa kuiwakilisha Serikali na taasisi zake, imeendesha mashauri ya uwekezaji katika miradi mikubwa ya kimkakati ya ujenzi wa reli ya kisasa, bwawa la maji la Mwalimu Nyerere, mashauri ya kikodi, nishati, madini, gesi na mashauri yenye maslahi mapana kwa taifa.
“OWMS ni mlinzi wa uchumi wa nchi yetu kulingana na majukumu tunayotekeleza kwa sababu pale tunaposhindwa kesi Serikali inalazimika kutoa fedha nyingi kulipa kesi husika,” amesema Dkt. Possi.
Akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa majukumu ya OWMS, Naibu Wakili Mkuu wa Serikali, Bi. Alice Mtulo alisema kuwa katika kipindi cha mwezi Julai, 2025 hadi Juni, 2026, OWMS imesajili jumla ya mashauri ya madai 3,069 yaliyoihusisha Serikali na taasisi zake ambapo katika kipindi husika mashauri 1,106 yalihitimishwa na kuokoa shilingi bilioni 438.6 kiasi ambacho Serikali ingelipa endapo ingeshindwa mashauri hayo.
Bi. Mtulo aliongeza kuwa katika kipindi cha mwezi Julai hadi Septemba, 2026 OWMS imesajili na kuendesha jumla ya mashauri ya madai 841, kuhitimisha mashauri 193 kati ya hayo na kuokoa shilingi bilioni 20.1.
Vile vile, Bi. Mtulo alisema kuwa kwa kipindi cha mwezi Julai, 2025 hadi Juni, 2026 OWMS imesajili jumla ya mashauri ya usuluhishi 81 yaliyoihusisha Serikali na taasisi zake, kuhitimisha mashauri 34 kati ya hayo na kuokoa shilingi bilioni 25.9 na dola za Marekani milioni 430.4 ambacho Serikali ingelipa endapo ingeshindwa mashauri hayo.
Aidha, katika kipindi cha mwezi Julai hadi Septemba, 2026, OWMS imesajili jumla ya mashauri 18 ya usuluhishi, kuhitimisha mashauri tisa (09) kati ya hayo na kuokoa dola za Marekani milioni 24.9, shilingi bilioni 1.6 euro 31,395 na paundi 1,304.50.
Kikao hicho kilihudhuriwa na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Mhe. Balozi Baraka Luvanda na wajumbe wa menejimenti ya OWMS.

.jpeg)



Post a Comment