Header Ads

test

TAKUKURU RUVUMA YAREJESHA MILIONI 44 ZA MIRADI TUNDURU NA NAMTUMBO

Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa TAKUKURU Mkoa wa Ruvuma imefanikiwa kurejesha Zaidi ya shilingi milioni 44.1 fedha za miradi katika Halmashauri za wilaya ya Tunduru na Namtumbo.

Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Ruvuma Hamza Mwenda akizungumzia utendaji kazi wa Taasisi hiyo katika kipindi cha kuanzia Aprili hadi Septemba 2026,amesema TAKUKURU imefanikiwa kurejesha kiasi hicho cha fedha kupitia ufutiliaji matumizi ya fedha za mradi wa ujenzi wa shule mpya ya msingi Majimaji wilayani Tunduru na mradi wa ujenzi wa vyumba sita vya madarasa katika shule ya msingi Mageuzi wilaya ya Namtumbo.

Mwenda amebainisha kuwa TAKUKURU wilaya ya Tunduru ilifanya uokoaji wa fedha Zaidi ya shilingi milioni 38.8 kiasi ambacho kilikuwa kimelipwa kwenda kwa Mzabuni Njowele Invstiment LTD aliyekabidhi mabati 227 ambayo yalikuwa chini ya kiwango.

Amesema baada ya ufuatiliaji uliofanywa na TAKUKURU kwa kushirikiana na Ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Tunduru pamoja na wasimamizi wa mradi na kuwekeana maazimio,mabati 227 yasiyo na ubora yaliondolewa na kuletwa mapya 227 yenye ubora unaotakiwa.

Amesema katika wilaya ya Namtumbo TAKUKURU ilifanya uokoaji wa fedha kiasi cha shilingi milioni 5.1 ambacho kilitakiwa kulipwa kwa mzabuni Bryce General Supply aliyewasilisha matofali yaliyokuwa chini ya kiwango.

Amesema baada ya ufuatiliaji wa TAKUKURU kwa kushirikiana na Ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Namtumbo matofali yasiyokuwa na ubora yaliondolewa na kuletwa matofali mapya yenye ubora unaotakiwa.

Katika hatua nyingine Mkuu huyo wa TAKUKURU Mkoa wa Ruvuma amesema TAKUKURU katika kipindi hicho ilifanya ufuatiliaji wa matumizi ya fedha za utekelezaji wa miradi ya maendeleo 31 yenye thamani ya shilingi bilioni 5.7 katika sekta za Utawala,miundombinu,afya na Elimu ili kuhakikisha thamani ya fedha inapatikana na utekelezaji wa miradi unalingana na fedha zilizotumika.

Hata hivyo amesema kati ya miradi 31 iliyotekelezwa,TAKUKURU imetoa mapendekezo ya kurekebisha mapungufu kwenye miradi 12 yenye thamani ya shilingi bilioni 2.2.

Akizungumzia uchunguzi wa mashitaka,Mwenda amesema TAKUKURU ilipokea malalamiko 118 kati ya hayo,malalamiko 85 yalihusu rushwa na 33 hayakuhusu rushwa na kwamba malalamiko yote yanayohusu rushwa uchunguzi umeanzishwa na upo katika hatua mbalimbali.

Ameyataja matarajio ya TAKUKURU katika kipindi cha Oktoba-Desemba 2026 kuwa ni pamoja na kuendelea kuelimisha na kuwashirikisha wananchi na wadau mbalimbali kwenye mapambano dhidi ya rushwa ili jamii ibadili mtazamo na kuichukia rushwa.

 

 

No comments