Header Ads

test

Wapiga kura 213,024 watarajia kushiriki Uchaguzi Mdogo Chamwino na Kata 11

Jumla ya wapiga kura 213,024 walioandikishwa katika Daftari la Kudumu la Wapiga Kura, wanatarajiwa kushiriki kwenye Uchaguzi Mdogo wa Ubunge katika Jimbo la Chamwino, Mkoa wa Dodoma na Udiwani katika Kata 11 za Tanzania Bara kesho tarehe 04 Novemba, 2026.

Takwimu hizo zimetolewa na Mwenyekiti wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) Mhe. Jaji (Rufaa) Jacobs C. M. Mwambegele wakati alisoma Risala ya Mwenyekiti kuhusu zoezi la kupiga kura kwenye uchaguzi huo.

Ametaja kati ya wapiga kura hao, wapiga kura 133,864 wapo kwenye Jimbo la Chamwino na wapiga kura 79,160 wapo kwenye kata 11 zitakazofanya uchaguzi mdogo na kwamba, jumla ya vituo 665 vya kupigia kura vitatumika, ambapo vituo 441 vipo kwenye Jimbo la Chamwino na vituo 224 vipo kwenye kata 11 zitakazofanya uchaguzi mdogo.

Mhe Jaji Mwambegele amezitaja kata 11 zinazofanya uchaguzi huo kuwa ni Nonde iliyopo Halmashauri ya Jiji la Mbeya; Lugenge, Halmashauri ya Mji Njombe; Bargish, Halmashauri ya Mji Mbulu; Makole, Halmashauri ya Wilaya ya Muheza na Mwera, Halmashauri ya Wilaya ya Pangani. 

Ameongeza kuwa, kata nyingine ni Oldonyosambu, Halmashauri ya Wilaya ya Ngorongoro; Igalula, Halmashauri ya Wilaya ya Uyui; Shelui, Halmashauri ya Wilaya ya Iramba; Mvumi, Halmashauri ya Wilaya ya Kilosa; Nyarero, Halmashauri ya Wilaya ya Tarime na Ilolangulu, Halmashauri ya Wilaya ya Mbogwe. 

“Kwa kuzingatia masharti ya kifungu cha 49(1)(b), (2) na (4), 57(2) na 68(2) vya Sheria ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani, Sura ya 343, kesho tarehe 04 Novemba, 2026 kutakuwa na uchaguzi mdogo wa Ubunge katika Jimbo la Chamwino, Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino, Mkoa wa Dodoma na Madiwani katika kata 11 za Tanzania Bara”, amefafanua Mhe. Jaji Mwambegele

Mhe. Jaji Mwambegele ameongeza kuwa katika uchaguzi huo, jumla ya wagombea 67 kutoka katika vyama vya siasa 17 wanawania nafasi wazi ya ubunge na udiwani katika Jimbo la Chamwino na kata 11 za Tanzania Bara, huku Jimbo la Chamwino likiwa na wagombea 16 wa nafasi ya Ubunge kati ya wagombea 08 sawa na asilimia 50 ni wanaume na wagombea 08 sawa na asilimia 50 ni wanawake. 

“Kata 11 zinazofanya uchaguzi mdogo wa udiwani zina jumla ya wagombea 51 ambapo kati ya hao wagombea 43 sawa na asilimia 84.31 ni wanaume na wagombea 08 sawa na asilimia 15.69 ni wanawake. Kwa namna ya pekee, Tume inavipongeza vyama vya siasa vinavyoshiriki na wagombea waliojitokeza kushiriki.”, amesema Mhe. Jaji Mwambegele.

Mhe. Jaji Mwambegele amevikumbusha vyama vya siasa vinavyoshiriki uchaguzi kesho tarehe 04 Novemba, 2026 kuzingatia wajibu wao wa kuweka mawakala katika vituo vyote vya kupigia, kuhesabia na kujumlishia kura na kwamba wasimamizi wa uchaguzi katika jimbo na kata husika, wamekamilisha taratibu zinazoweka mazingira yanayowawezesha mawakala wa vyama vya siasa kufuatilia mchakato mzima wa uchaguzi.

“Mawakala hao, wanawajibika kuwakilisha na kulinda maslahi ya vyama na wagombea wao. Hivyo, wanapaswa kuzingatia Sheria, Kanuni, taratibu za uchaguzi na maelekezo ya Tume katika utekelezaji wa majukumu yao vituoni.”, amefafanua Mhe. Jaji Mwambegele.

Mwenyekiti huyo wa INEC amevikumbusha vyama vya siasa, wagombea, mawakala, wapiga kura na wananchi wote kwa ujumla kuzingatia kuwa mpiga kura, anatakiwa kwenda katika kituo alichojiandikisha na kadi yake ya mpiga kura siku ya uchaguzi.

“Wapiga kura watakaoruhusiwa kupiga kura ni wale walioandikishwa katika Daftari la Kudumu la Wapiga Kura. Mpiga kura awapo kituoni anatakiwa kutoa kipaumbele kwa wapiga kura wenye mahitaji maalumu kama vile wazee, wagonjwa, watu wenye ulemavu, wajawazito na akina mama wenye watoto wachanga watakaokuwa nao kituoni.”, amesema Mhe. Jaji Mwambegele na kuongeza kuwa;

“Watu wenye mahitaji maalumu wanaruhusiwa kwenda kituoni na wasaidizi wao.

”Vituo vitafunguliwa saa 01:00 asubuhi na kufungwa saa 10:00 jioni. Ifikapo muda wa kufunga kituo saa 10:00 kamili jioni, kama wapiga kura bado wapo kwenye mistari, mlinzi wa kituo atasimama nyuma ya mtu wa mwisho na zoezi la upigaji kura litaendelea hadi wapiga kura waliopo kwenye mstari watakapomalizika. Mpiga kura atakayefika zaidi ya muda wa kufunga kituo hataruhusiwa kupiga kura.

”Baada ya kumaliza kupiga kura, mpiga kura anatakiwa kuondoka eneo la kituo cha kupigia kura; na Mpiga kura awapo kituoni, anatakiwa kufuata maelekezo yote atakayopewa na karani mwongozaji wapiga kura”.

Mhe. Jaji Mwambegele amesisitiza kuwa kwa kuzingatia masharti ya kifungu cha 4, 14(2), 19(3), 84(3)(a) na (b) na 164 vya Sheria ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani, Sura ya 343, vikisomwa pamoja na kifungu cha 26 cha Sheria ya Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, Sura ya 292, Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, ilitoa maelekezo ya kisera katika Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2025.

Ameyataja maelekezo hayo kwamba, kwa mpiga kura asiye na picha katika Daftari la Kudumu la Wapiga Kura lakini ana kadi ya Mpiga Kura yenye taarifa binafsi zilizomo katika Daftari la Kudumu la Wapiga Kura, ARUHUSIWE KUPIGA KURA;

”Kwa mpiga kura ambaye ana kadi yenye namba ya mpiga kura inayotofautiana na namba ya mpiga kura iliyomo katika Daftari la Kudumu la Wapiga Kura lakini taarifa nyingine zote ikiwemo picha na majina yaliyopo katika Daftari la Kudumu la Wapiga Kura ni sawa kama ilivyo katika kadi ya mpiga kura aliyonayo; ARUHUSIWE KUPIGA KURA”, ameongeza Mhe. Jaji Mwambegele na kuongeza kuwa:

”Kwa mpiga kura ambaye ameandikishwa katika Daftari la Kudumu la Wapiga Kura na taarifa zake zipo katika Daftari la Kudumu la Wapiga Kura lililopo katika kituo husika, lakini amepoteza kadi yake au kadi yake imeharibika, ARUHUSIWE KUPIGA KURA kwa kutumia vitambulisho vifuatavyo;-

a) Kitambulisho cha Taifa (NIDA); 

b) Leseni ya udereva; au 

c) Pasi ya kusafiria (Passport).

Ametaja sharti la maelekezo hayo kuwa, majina yake yaliyopo katika kitambulisho atakachowasilisha mpiga kura, ni lazima yafanane na majina yote kama yalivyo katika Daftari la Kudumu la Wapiga Kura.

Aidha amefafanua kuwa, kwa mpiga kura ambaye ana kadi ya kupigia kura lakini taarifa zake hazipo katika Daftari la Kudumu la Wapiga Kura ASIRUHUSIWE KUPIGA KURA.


Mhe. Jaji Mwambegele amewakumbusha wadau wote kuzingatia maelekezo haya ya kisera na kwamba ametoa rai kwa wapiga kura kwenye maeneo yenye uchaguzi, kujitokeza kwa wingi kwenye vituo vya kupigia kura hapo kesho ili kuwachagua viongozi wanaowataka.

No comments