Header Ads

test

Maadili ya viongozi wa umma yawe kipaumbele kwa vyombo vya habari


Ofisi ya Rais, Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma Kanda Maalum imefanya kikao kazi na wadau wa habari, wakiwemo wamiliki, wahariri na waandishi wa habari, kwa lengo la kujenga ushirikiano endelevu kati ya taasisi hiyo na vyombo vya habari nchini.


Kikao kazi hicho kimefanyika Aprili 9, 2026 katika ukumbi wa mikutano wa Shule ya Uongozi Mwalimu Nyerere, Kibaha, mkoani Pwani.

Akifungua kikao hicho, Katibu Msaidizi wa Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma Kanda Maalum, Bi. Elizabeth Komba, amesema vyombo vya habari si kioo tu cha jamii bali pia ni nyenzo muhimu ya kuunda na kukuza maadili nchini.

“Tunaamini kuwa vyombo vya habari vina nafasi ya kipekee katika kukuza maadili, uwajibikaji na uwazi katika jamii. Kwa maneno mengine, nyinyi ni nguzo muhimu katika kujenga au kubomoa maadili katika jamii. Hivyo, tutumie tasnia hii kujenga jamii yenye uadilifu,” amesema Bi. Komba.

Aidha, ameongeza kuwa vyombo vya habari vina nafasi kubwa katika kukuza uwajibikaji kwa kufichua vitendo vya rushwa, ubadhilifu na matumizi mabaya ya madaraka, kwa kuweka wazi ukweli unaowezesha wahusika kuwajibika.

“Kama tukitumia vyombo vya habari kwa njia sahihi, tunaweza kujenga jamii yenye uadilifu, uwazi na haki. Lakini tukivitumia vibaya, tunaweza kuharibu maadili, kuleta migawanyiko miongoni mwetu na hatimaye kujenga jamii isiyo na uzalendo,” alisisitiza.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Mipango, Ufuatiliaji na Tathmini kutoka Sekretarieti hiyo, Bw. Omary Juma, amesema ushirikiano huo utakuwa endelevu, huku wakiahidi kuendelea kukutana mara kwa mara ili kujadili mbinu bora za kukuza na kuimarisha maadili nchini.

Katibu Msaidizi Ofisi ya Rais, Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma Kanda Maalum Bi. Elizabeth Komba akizungmza wakati akifungua Kikao Kazi cha wamiliki, wahariri na waandishi wa habari wa Kanda hiyo. Kikao hicho kimefanyika katika ukumbi wa mikutano wa Shule ya Uongozi Mwalimu Nyerere mjini Kibaha mkoani Pwani tarehe 09 Aprili, 2026.





 

No comments