Tanzania yaendelea kuwa Shule ya Utumishi Barani Afrika, Ridhiwani Kikwete awapokea Wasomali 25
Na: Jawadu Kinyobwa
Tanzania imezidi kujiimarisha kama kitovu cha mafunzo utawala bora barani Afrika baada ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Ridhiwani Kikwete, kupokea ujumbe wa watu 25 kutoka nchini Somalia kwa ajili ya programu maalumu ya mafunzo ya kuendesha shughuli za utumishi wa umma kwa ufanisi.Akizungumza mara baada ya kuwakaribisha wajumbe hao Aprili 28 , Mhe. Kikwete ameeleza kuwa ujio huo ni kielelezo cha imani ambayo mataifa mengine wanayo kwa Tanzania kama nchi ya mfano katika kuimarisha amani, utulivu na maendeleo ya kiutawala.
Amesema lengo kuu la ugeni huo ni kujifunza namna mifumo ya utumishi wa umma nchini inavyofanya kazi, ikiwemo usimamizi wa rasilimali watu na namna utumishi huo unavyoweza kujibu kero za wananchi kwa haraka na usahihi.
Waziri Kikwete amesisitiza kuwa Watanzania wapaswa kujua kwamba "wamekalia dhahabu" kutokana na mabadiliko makubwa ya kimfumo yaliyofanyika, hususan katika kipindi cha Serikali ya Awamu ya Sita inayowezesha wananchi kuwasiliana moja kwa moja na serikali yao.
Amebainisha kuwa matumizi ya teknolojia (Digitalization) yamerahisisha huduma ambapo kwa sasa mtumishi wa umma hahitaji kusafiri kutoka mkoani kwenda Dodoma kufuata huduma, bali anaweza kupata mahitaji yake, ikiwemo maombi ya mikopo na mawasiliano na viongozi, kupitia mifumo ya kidijitali iliyowekwa.
Kwa upande wake, Kaimu Katibu Mkuu ambaye pia Naibu Katibu Mkuu wa ofisi hiyo, Bw. Xavier Daudi, amefafanua kuwa wajumbe hao watapitishwa kwenye maeneo muhimu ya kiutendaji ikiwemo muundo wa serikali, mifumo ya Serikali Mtandao (e-Government), na mbinu za kisasa za utunzaji wa nyaraka.
Amesema upekee wa mifumo ya Tanzania na miundombinu yake ya kisasa ya kiutendaji ndivyo vinavyovutia nchi nyingi za Afrika Mashariki na kwingineko kuja kujifunza.
Awali akizungumza Mkuu wa Chuo na Mtendaji Mkuu wa Chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania (TPSC), Ernest Mabonesho, ambaye ndiye mratibu wa programu hiyo, amebainisha kuwa mafunzo hayo ni matokeo ya makubaliano yaliyofikiwa mwaka 2025 kupitia Wizara ya Mambo ya Nje.
Amesema zoezi hilo ni muendelezo wa ushirikiano wa kihistoria kati ya Tanzania na Somalia, wenye lengo la kujenga kuwezesha serikali kufanya kazi kwa tija na kwa manufaa ya mataifa yote mawili.
Naye, mmoja wa washiriki wa mafunzo hayo kutoka Somalia, Ayan Andullahi ameeleza kuwa kupitia mafunzo hayo amejifunza kwa kina kuhusu namna Tanzania ilivyofanikiwa kujenga mifumo madhubuti ya utumishi wa umma inayozingatia uwajibikaji, uwazi na utoaji wa huduma ufanisi na kwa wakati.


.jpeg)




Post a Comment