Na Mwandishi Wetu
Weledi, maadili na uelewa wa sheria kwa waandishi wa habari vimetajwa kuwa nyenzo muhimu katika kulinda haki za wananchi na kuhakikisha jamii inapata taarifa sahihi kuhusu masuala ya kisheria, haki za binadamu na ukatili wa kijinsia.
Hayo yameelezwa na Mjumbe wa Bodi ya Ithibati ya Waandishi wa Habari (JAB), Wakili Ladislaus Komanya, tarehe 09 Juni 2026 wakati akiwasilisha mada kuhusu "Uhuru wa Vyombo vya Habari katika Enzi ya Kidijiti: Wajibu wa Bodi ya Ithibati ya Waandishi wa Habari" katika mafunzo ya waandishi wa habari yaliyoandaliwa na Wizara ya Katiba na Sheria wilayani Tarime, mkoani Mara.
Wakili Komanya amesema uhuru wa vyombo vya habari unaenda sambamba na uwajibikaji wa mwandishi katika kuthibitisha taarifa, kuzingatia maadili ya taaluma na kuheshimu sheria za nchi.
Ameongeza kuwa waandishi wa habari wanapaswa kutumia fursa zinazotolewa na teknolojia za kidijiti kwa kuzingatia weledi na maadili ili kuhakikisha taarifa wanazozitoa zinachangia upatikanaji wa haki, maendeleo ya jamii na ustawi wa wananchi.
"Mwandishi wa habari anapaswa kuzingatia misingi ya taaluma, maadili na sheria ili kuhakikisha taarifa anazozitoa zinachangia upatikanaji wa haki na maendeleo ya jamii," amesema Wakili Komanya.
Aidha, amesisitiza umuhimu wa waandishi wa habari kuthibitisha taarifa kabla ya kuzichapisha au kuzirusha, hususan wanaporipoti masuala yanayohusu sheria, haki za binadamu na makundi maalumu katika jamii.
Amesema matumizi ya teknolojia za kidijiti yanapaswa kwenda sambamba na uwajibikaji ili kulinda hadhi ya taaluma ya habari na maslahi ya umma.
Akifungua mafunzo hayo, Mkuu wa Wilaya ya Tarime, Meja Edward Gowele, amesema mafunzo hayo yataongeza tija katika utoaji wa habari za kisheria na kusaidia wananchi kutambua haki zao kupitia vyombo vya habari.
Amesema pia kuwa ongezeko la matukio ya ukatili wa kijinsia yanayoripotiwa katika vyombo vya sheria linahitaji ushiriki mkubwa wa waandishi wa habari katika kutoa elimu na taarifa sahihi kwa wananchi ili kusaidia juhudi za kuyatokomeza.
"Endapo mtatumia mafunzo haya kwa ufasaha, yataongeza tija katika kuhabarisha wananchi kuhusu mafanikio ya huduma za msaada wa kisheria pamoja na changamoto zinazojitokeza katika jamii zetu," amesema Gowele.

Kwa upande wake, Mratibu wa mafunzo hayo kutoka Wizara ya Katiba na Sheria, Wakili wa Serikali Athumani Msosole, amesema mafunzo hayo yatawawezesha waandishi wa habari kutambua namna bora ya kuripoti masuala ya ukiukwaji wa haki za binadamu, changamoto za kisheria pamoja na hatua zinazochukuliwa na mamlaka mbalimbali katika kutatua matatizo hayo ndani ya jamii.
Msosole amesema uandishi sahihi wa habari za masuala ya sheria una mchango mkubwa katika kuongeza uelewa wa wananchi kuhusu haki zao na huduma mbalimbali za msaada wa kisheria zinazotolewa nchini.
Naye Mwenyekiti wa Chama cha Wanahabari Tarime, Jacob Karoli, amesema mafunzo hayo yamekuja wakati muafaka kwani yatawajengea waandishi wa habari uwezo wa kuandika habari za kisheria kwa usahihi zaidi na hivyo kuongeza manufaa ya habari hizo kwa wananchi.
Jumla ya waandishi wa habari 40 kutoka Wilaya ya Tarime wanashiriki mafunzo hayo yanayolenga kuwawezesha kuwa mabalozi wa elimu ya sheria, haki za binadamu na mapambano dhidi ya ukatili wa kijinsia katika maeneo yao.





Post a Comment