IMANI YA JUMUIYA YA KIMATAIFA KWA UONGOZI WA RAIS SAMIA IMEJIDHIHIRISHA KUPITIA UFADHILI WA DOLA BILIONI 1.277 KUENDELEZA UJENZI WA SGR.
Aprili 28, 2026, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imesaini mkataba wa kukamilisha mpango wa ufadhili wa pamoja wenye thamani ya takribani dola za Marekani bilioni 1.277 kwa ajili ya kuendeleza ujenzi wa Reli ya Kisasa (SGR), kipande cha tatu (Lot 3) na cha nne (Lot 4) kutoka Makutupora hadi Isaka.
Ufadhili huu mkubwa unaotolewa kwa ushirikiano wa taasisi za dhamana za mikopo ya mauzo ya nje kutoka Italia (SACE), Sweden (EKN) na Poland (KUKE), ukiratibiwa na Benki ya Standard Chartered, ni zaidi ya ufadhili na ni alama ya imani ya kimataifa kwa uongozi thabiti wa Tanzania chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Imani ya Jumuia ya Kimataifa Imejengwa Katika Utekelezaji
Imani ya Jumuia ya Kimataifa Imejengwa Katika UtekelezajiKatika diplomasia ya maendeleo, fedha hufuata imani. Mataifa na taasisi za fedha za kimataifa hutoa rasilimali pale tu zinapoona uthabiti wa kisera, uwazi wa uongozi, na uwezo wa utekelezaji wa miradi mikubwa.
Kupatikana kwa ufadhili huu ni ushahidi kwamba jumuiya ya kimataifa inaamini katika dira ya maendeleo ya Tanzania, hasa katika sekta ya miundombinu ya reli ambayo ni mhimili wa ukuaji wa uchumi wa kisasa.
Mwaka 2021, Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, alipoingia madarakani, kwa uwazi aliuahidi Umma wa Watanzania kwamba Serikali yake haitasimamia tu na kukamilisha vipande vya SGR vilivyoanza kutekelezwa na mtangulizi wake, bali pia kuanzisha vipande vipya ili kuhakikisha Tanzania inaunganika kwa reli ya kiwango cha kimataifa kutoka bandari hadi nchi jirani. Leo ahadi hiyo si nadharia tena bali ni utekelezaji usiyohitaji sayansi ya roketi kuuona.
Ahadi Imetafsiriwa Kwa Vitendo
Chini ya uongozi wake, kipande cha Dar es Salaam–Morogoro kimekamilika na kuanza kutoa huduma ya treni za umeme kati ya Dar es Salaam na Dodoma tangu Juni 2024 na kuonyesha mafanikio yaliyoweka historia mpya ya usafiri katika sekta ndogo ya reli nchini.
Aidha kwa mujibu wa Meneja wa mradi wa kipande cha pili kati ya Morogoro na Makutopora, Mhandisi Kelvin Kimambo, kipande hicho kimefikia asilimia 98.7 ambapo utandikaji wa reli na mifumo yake ya uendeshaji (umeme) , imekamilika mpaka Makutopora na kwamba kinachoendelea sasa ni umaliziaji kazi za mifumo ikiwemo pia kazi za ujenzi wa uzio.
Katika hatua nyingine Mhandisi Kimambo, amesema, TRC inatarajia kufungua treni ya mizigo kati ya Dar Es Salaam na Bahi mwishoni mwa mwezi Mei 2026.
Kuna msemo wa Wazaramo unaosema zilongwa mbali na zitendwa mbali (yaani kusema na Kutenda ni vitu viwili tofauti) lakini kwa Rais Daktari Samia, hali ni tofauti, aliahidi na ametekeleza (Walk the Talk).
Ufadhili Huu Ni Kura ya Imani kwa Tanzania
Ni muhimu Watanzania kuelewa kuwa taasisi kama SACE, EKN na KUKE hutoa dhamana za mikopo baada ya tathmini pana ya uwezo wa nchi husika unaojikita katika kuangazia uimara wa uchumi, usimamizi wa deni, na mazingira ya uwekezaji.
Kwa taasisi hizi kuingia kwenye mpango wa pamoja wa zaidi ya dola bilioni 1.277 si jambo la kawaida, hii ni KURA YA IMANI KWA TANZANIA.
Aidha, uratibu wa Benki ya Standard Chartered katika mpango huu unaonesha pia sekta ya fedha ya kimataifa inaiona Tanzania kama mshirika mwenye kuaminika katika utekelezaji wa miradi mikubwa ya kimkakati.
SGR Kama Mradi wa Kimkakati wa Kikanda
Kipande cha Makutupora hadi Isaka si mradi wa ndani pekee, ni sehemu ya mtandao mpana unaolenga kuifanya Tanzania kuwa kitovu cha usafiri na biashara katika Afrika Mashariki na Kati.
Kupitia SGR, bandari ya Dar es Salaam inaendelea kuimarishwa kama lango la biashara kwa nchi zisizo na bandari kama Rwanda, Burundi, DRC, Uganda na Zambia.
Hivyo, ufadhili huu pia ni uthibitisho kuwa dunia inaamini nafasi ya Tanzania kama mhimili wa uchumi wa kikanda.
Uongozi wa Rais Samia na Diplomasia ya Uchumi
Mafanikio haya hayawezi kutenganishwa na diplomasia ya uchumi ya Daktari Samia, ambayo imeongeza ushirikiano wa kimataifa, kuimarisha uhusiano na washirika wa maendeleo na kuongeza mvuto wa Tanzania kwa wawekezaji na taasisi za fedha.
Kwa mtazamo huu, ufadhili wa SGR si tu matokeo ya mahitaji ya mradi, bali ni zao la kuaminika kwa sera, utawala na uongozi wa serikali ya awamu ya sita, inayoongozwa na Rais Samia.
Kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu,
Imeandaliwa na kitengo cha Uhusiano na Mawasiliano,
Shirika la Reli Tanzania (TRC)

.jpeg)
.jpeg)

Post a Comment