Header Ads

test

Kijana wa Mtwara Avunja Ukimya wa Hedhi Salama



Na: Mohammed Hammie

Wakati masuala ya hedhi yakiendelea kuzungumzwa kwa sauti ya chini katika jamii nyingi, kijana mmoja kutoka kijiji cha Lipwidi mkoani Mtwara ameamua kuvunja ukimya huo, na cha kushangaza zaidi, yeye ni mwanaume.

Makungu Mrope (24), anayejulikana kwa jina la utani “Kaka wa Hedhi”, anajitolea kutoa elimu ya hedhi salama kwa wasichana, wanawake na hata wanaume katika jamii yake. Kupitia juhudi zake, anabadilisha mtazamo uliokita mizizi kwamba hedhi ni suala la siri linalowahusu wanawake pekee.

Safari ya Mrope ilianza tangu utotoni, baada ya kushuhudia tukio lililomuacha na maswali mengi. Dada yake alipata hedhi akiwa shuleni wakati wa mapumziko na kukumbana na dhihaka kutoka kwa wanafunzi wenzake.

“Walianza kumzomea na kuimba kuwa amechinja kuku. Ilikuwa aibu kubwa sana,” anasimulia Mrope.

Anasema wakati huo hakuelewa kilichotokea hadi alipofuatilia baada ya siku chache. Kilichomuumiza zaidi ni kuona dada yake akizuiwa kwenda shule kwa wiki nzima kutokana na tukio hilo.

“Tukio lile liliniumiza sana. Ndipo nikaweka nia kwamba nitakapokuwa mkubwa nitaelimisha kuhusu hedhi salama ili wasichana wasipitie mateso kama yale,” anasema.

Baada ya kushindwa kuendelea na masomo ya juu ya sekondari, Mrope aligeukia kujielimisha kupitia zahanati ya kijiji na machapisho ya Wizara ya Afya. Hatimaye alianza kutoa elimu hiyo kwa jamii yake.

Juhudi zake zilitambuliwa na uongozi wa kijiji cha Lipwidi, uliompa kibali cha kuendesha shughuli zake rasmi za uelimishaji. Tangu hapo, amekuwa akitembelea shule mbalimbali kutoa elimu ya hedhi salama.

Kila asubuhi, Mrope huanza siku yake kwa kutembelea shule ya sekondari aliyosoma, ambapo hupata dakika 30 wakati wa gwaride la asubuhi kuzungumza na wanafunzi. Katika vipindi hivyo, hutoa elimu na kujibu maswali mbalimbali kutoka kwa wanafunzi.

“Sifanyi kazi hii peke yangu. Mara nyingi nashirikiana na wataalamu wa afya kutoka zahanati ya kijiji,” anasema.

Mbali na shughuli za uelimishaji, Mrope pia anajishughulisha na biashara ya kuuza nguo za kiume. Hata hivyo, dukani kwake pia hupatikana taulo za kike (pedi), jambo lisilo la kawaida kwa wafanyabiashara wengi wa aina hiyo.

Anasema kila mteja anayenunua bidhaa hiyo hupata pia elimu ya matumizi sahihi na umuhimu wa usafi wa hedhi.

Mrope anaamini kuwa wanaume wana nafasi muhimu katika kubadili mtazamo wa jamii kuhusu hedhi.

“Ninapenda kuwaelimisha wanaume wenzangu kuhusu umuhimu wa hedhi kwa wanawake na wasichana. Wengi wameanza kubadilika,” anasema.

Anaongeza kuwa ushiriki wa wanaume unaweza kusaidia kuondoa unyanyapaa, kuboresha afya ya uzazi, na kuongeza uelewa sahihi kuhusu hedhi kama suala la kiafya badala ya aibu au siri.

Wakati dunia ikiadhimisha Siku ya Hedhi kila mwaka tarehe 28 Mei, jitihada za Mrope zinaakisi lengo la siku hiyo, kuongeza uelewa, kuondoa unyanyapaa, na kuhakikisha upatikanaji wa vifaa salama vya hedhi kwa wasichana na wanawake.

Kwa kupitia kazi yake, “Kaka wa Hedhi” anaendelea kuwa sauti muhimu ya mabadiliko katika jamii, akionesha kuwa elimu ya hedhi salama ni jukumu la kila mtu, bila kujali jinsia.


No comments